07 September 2012

Wawekezaji washauriwa kujiunga na Soko la Mitaji


Na Hyasinta Timothy

WAWEKEZAJI, kampuni mbalimbali  za ndani zimeshauriwa kujiunga katika Soko la Mitaji ili kusaidia kukuza mtaji wa Soko la Hisa, hatua itakayosaidia kutoa mkopo kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya nchi.

Ushauri huo ulitolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Ramadhani Khijah katika kongamano la Kukuza Soko la Mitaji lililofanyika jana  jijini Dar es Salaam na kuratibiwa na Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), IFC na Benki ya NIC

Alisema ili kutekeleza sera za maendeleo lazima tujipange ili tuweze kutumia soko la hisa kwa ajili ya kusaidia miundombinu ya barabara, umeme na masuala mengine ya maendeleo kwa njia ya kutoa mikopo.

"Viwanda, mashirika mbalimbali, kampuni za simu, wawekezaji wadogo, kati na wakubwa, wawekeze katika soko la mitaji na si wawekezaji kutoka nje hatua itakayosaidia kukuza mtaji kutokana na dhamana yao," alisema na kuongeza

"Naelewa waratibu wamewashirikisha wadau zaidi ya 100 kutoka kampuni, taasisi mbalimbali kwa ajili ya kujadili mikakati ya kuweza kukuza soko la hisa kwa manufaa ya Tanzania,"alisema.


Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bi.Nasama Massinda alisema wameshapeleka mapendekezo serikalini kuwa masoko ya mitaji kupata mitaji kutoka kwa wafanyabiashara wadogo na serikali za mitaa kupata mitaji ili wapate mikopo kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo.

"Wale wawekezaji waliojiunga  nje ya nchi warudi nyumbani Tanzania wajiunge na soko la mitaji ili kukuza mtaji wa Soko la Hisa ili tuweze kuleta maendeleo zaidi,"alisema.

2.
'Sheria mpya ya wavuvi inatuumiza'
Na Wilhelm Mulinda,
Mwanza

WAFANYABIASHARA wa Soko la Mwaloni Kirumba jijini Mwanza wameiomba serikali kufuta, Sheria mpya ya Uvuvi ya mwaka 2012 kwa madai kuwa haina manufaa kwa wananchi na inaongeza umaskini kwa watu wenye kipato kidogo.

Akizungumza na Majira jijini hapa jana, Mwenyekiti wa umoja wa wafanyabiashara hao, Bw. Christopher Richard, alisema kuwa Sheria hiyo (Laboratory Fees Regulations,
2012), maandalizi yake hayakuhusisha wadau wa soko hilo.

Bw. Richard alisema kuwa katika sheria hiyo ambayo ilianza kutumika kuanzia Julai mosi, mwaka huu, inamtaka mfanyabiashara kulipia kibali sh. 50,000 kwa ajili ya kusafirisha samaki pamoja na mazao ya uvuvi kutoka katika soko hilo kwenda sehemu
zingine nchini, ambapo kabla ya hapo kibali hicho kilikuwa kinatolewa bure.

Alisema kuwa sheria hiyo haizingatii wingi au uzito wa samaki wanaosafirishwa isipokuwa inataka kila anayesafirisha samaki pamoja na mazao ya uvuvi kulipia kibali cha sh. 50,000.

"Lengo la serikali ni kusaidia wananchi wake. Hivyo kutoka shilingi sifuri hadi sh.50,000 ni kuwakandamiza wananchi na kuwaongezea umaskini watu wenye kipato kidogo", alisema.

Aidha mwenyekiti huyo alisema kuwa katika sheria hiyo mpya ya uvuvi, usajili wa mitumbwi nao unatakiwa kulipiwa sh. 50,000 badala ya kiwango cha zamani ambacho kilikuwa ni sh. 15,000

"Katika sheria mpya, malipo yanatakiwa kufanyika katika maabara ya samaki iliyopo Nyegezi jijini hapa hali ambayo inasababisha usumbufu kwani mvuvi au mfanyabiashara anahitaji kusafiri umbali mrefu ili kupata huduma.

Alishauri maabara hiyo ya samaki kukusanya ushuru kwa wateja wanaokwenda kupimiwa sampuli za samaki kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi na huduma zingine ziendelee
kutolewa katika halmashauri za wilaya ili kuwasogezea wananchi karibu.

Pia katika sheria hiyo mpya ya  uvuvi, mtu anayetaka kuanzisha ufugaji wa samaki anatakiwa kulipa sh. 100,000 hali ambayo inaweza kuvunja moyo watu wanaotaka kufanya hivyo kutokana na kiwango cha malipo kuwa kikubwa.

Alisema kuwa serikali ikihamasisha wananchi kufuga samaki, hali hiyo itasaidia kukabiliana na upungufu wa samaki katika maziwa na sehemu nyingine.


3.
Mradi wa 'NMB Financial Fitness' wakubalika

Na Darlin Said

MRADI wa Benki ya NMB unaofahamika kama utunzaji wa  akiba kwa wanafunzi 'financial fitness' umefikia katika hatua za mwisho katika Kanda ya Kusini. 

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kutoka Benki ya NMB ilieleza mradi huo ulianza Mei, mwaka huu na sasa umeshafika  Mtwara, Lindi na Ruvuma.

Ilieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa mradi huo ambao ulilenga uwekaji wa akiba kwa vijana  umeshafika katika shule za msingi zaidi ya 45,000 nchi nzima.

Ilieleza pia  mradi  huo umezifikia shule 20 katika Mkoa wa Lindi, Mtwara na Ruvuma.

"Mradi huu umekubalika kwa wanafunzi ambao walijiunga na  mradi huu Mkoa wa Mtwara," alisema na kuongeza kuwa wengi wao walisema wameshaanza kujitahidi kuweka akiba zao kwa ajili ya malengo yao ya muda mrefu na mfano mzuri ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Liwale, Idrissa Ndumbaro ambaye alieleza kuwa ameshaanza kuweka akiba ya fedha zake kwa ajili ya kuja kujenga nyumba," ilieleza.


Benki hiyo iliwapongeza wanafunzi wote walioanza utaratibu wa kuweka akiba kwani hatua hiyo itawasaidia kuweza kutambua na kuwa na uelewa wa fedha kwa asilimia kubwa.

Ilielezwa kuwa NMB ilitambua umuhimu wa kuweka akiba kwani wanafunzi wakianza kuweka akiba wakati wapo shule, utaratibu huo  utwasaidia kuwa na maarifa ya ziada kuhusu utunzaji wa akiba.

No comments:

Post a Comment