26 September 2012

CHADEMA acheni kumsusia Tendwa-CCK


Na Goodluck Hongo

CHAMA cha Demokradia na Maendeleo (CHADEMA), kimetakiwa kuacha kususia shughuli zinazofanywa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Bw. John Tendwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Bw. Renatus Muabhi, aliyasema hayo Dar es Salaam jana na kuongeza kuwa, CHADEMA hakikutumia busara na haki ya kikatiba kususia semina ambayo ilishirikisha Jeshi la Polisi na vyama vya siasa.

Alisema lengo la semina hiyo ni kujadili vifo vilivyotokea katika mikutano ya chama hicho ambacho kina ushindani mkubwa wa kisiasa hivyo hakuna sababu ya kuigomea Serikali.

Alisema makubalino waliyofikiwa katika semina hiyo ni vyama vyote kuhakikisha hakuna vurugu zinazotokea katika mikutano yao na kama zitatokea, chama husika kitachukuliwa hatua.

Aliongeza kuwa, Jeshi la Polisi limekubali kubadilika ambapo mambo mengine yaliyotokea ni makosa ya kibinadamu hivyo mkutano huo ulikuwa na malengo mazuri.

“Ibara ya 18 ya katiba ya nchi inasema, kususia mjadala wa kitaifa si kitu kizuri, nampongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema na Bw. Tendwa kwa kubadilishana mawazo na viongozi wa vyama vya siasa pamoja na kujadili kwa kina umuhimu wa amani na usalama wa nchi yetu,” alisema.

Bw. Muabhi alisema vyama vya siasa na wanasiasa watapita lakini nchi haitapita bali itaendelea kuwepo ambapo CCK wana kiongozi mzuri na maarufu nchini ambaye wanasubili wakati ukifika atajitokeza.

“Kiongozi huyu akishajitokeza, watu wengi wataikataa CHADEMA na kujiunga CCK,” alisema Bw. Muabhi.

Akijibu madai hayo, Ofisa Habari wa CHADEMA, Bw. Tumaini Makene, alisema chama hicho hakina muda wa kujibizana na CCK wala kupotezewa lengo la wajibu wao kwa Watanzania.

Alisema Watanzania wanaendelea kuwaamini kwa kuongoza vuguvugu la mabadiliko makubwa ya kimfumo na kiutawala.

“CCK inashikia bango jambo wasilolijua na kufanya propaganda zenye lengo la kupotosha na kuficha ukweli, wanazidi kujifunua sura zao halisi kuwa wapo kwa ajili ya masilahi ya nani, sisi hatukujua kuma semina iliyoitishwa na Bw. Tendwa, msemaji wake ni CCK.

“Wananchi watajionea mzunguko wa propaganda za vyombo vya sola, CCM na Serikali yake ulivyo, CCK imetumwa kusemea semina ya Bw. Tendwa lakini Bw. Muabhi hawezi kuwasemea Watanzania wanaodai haki na uwajibikaji kwa ustawi wa nchi yao,” alisema.

No comments:

Post a Comment