26 September 2012
Ma DC waagizwa kutenga maeneo ya waathirika Dar
Na David John
WAKUU wa Wilaya, Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, wameagizwa kuandaa na kutenga maeneo yatakayotumika kuwahifadhi watu ambao wataathirika na mafuriko.
Mkuu wa Mkoa huo Bw. Meck Sadick, aliyasema hayo Dar es Salam jana katika Kikao cha Kamati ya Maafa Mkoa ambacho kiliwakutanisha viongozi hao.
Washiriki wengine katika kikao hicho ni Wakurugenzi na Maofisa wa Halmahsuli za Kinondini, Temeke na Ilala ili kupanga mikakati ya kukabiliana na mafuriko yanayoweza kutokea kuanzia Oktoba mwaka huu.
“Safari hii sitaki kuona watu wanapelekwa katika shule ili kupatiwa hifadhi, nawataka mtenge maeneo mapema kwa ajili ya tahadhali kwani hatujui ya Mungu,” alisema Bw. Sadick.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imehadharisha kutokea mafuriko makubwa kuanzia Oktoba mwaka huu hivyo lazima maandalizi yawekwe mapema badala ya kusubili tukio litokee.
Alisema mbali ya kutenga maeneo hayo, halmashauri hizo chini ya Wakurugenzi wake zihakikishe zinatenga fedha za dharula ambazo zitaweza kusaidia wananchi ambao wataathirika.
“Sio kila kitu kitoke Ofisi ya Mkuu wa Mkoa au Waziri Mkuu, hata unga kilo kumi nazo zitoke katika ofisi zetu, tengeni fedha za kuhudumia wananchi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Bw. Sadick alisema kwa muda mrefu Mkoa huo ulikosa chombo ambacho kitashughulikia matukio mbalimbali mkoani humo ambapo hivi sasa, wamekianzisha na kukipa jina la DARMART, ili kusimamia majanga yanayotokea.
Alisema chombo hicho kimeshirikisha makundi mbalimbali ya watalaamu ili kuleta ufanisi wa kupambana na matuko hususan changamoto za marufiko.
Aliwataka wananchi hasa waishio mabondeni kuchukua tahadhali kabla ya hatari kwa kusafisha, kuzibua mitaro na mifereji ambayo inachangia maji kufurika na kusambaa katika makazi ya watu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment