10 September 2012
Bodaboda kupewa mafunzo usalama barabarani nchini
Na Rehema Maigala
JESHI la Polisi nchini linaanzisha mafunzo kwa waendesha pikipiki (bodaboda)ili kupunguza ajali za barabarani na ualifu unaotokea mara kwa mara.
Mafunzo hayo ambayo yanaanzia jijini Dar es Salaam baada ya jeshi hilo kupata mfadhili wa kuwezesha kuwafundisha waendesha pikipiki hao sheria za barabarani na jinsi ya kuendesha pikipiki kwa usalama.
Akizungumza katika ofisi za gazeti la majira Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Nchini (SSP) Saimon Ngowi,alisema kuwa kuwa mafunzo hayo yatachukua waendasha pikipiki watakaotoka Wilaya tatu za jijini Dar es Salaam ambazo ni, Temeke, Ilala na Kinondoni.
Alisema kuwa jumla ya waendesha pikipiki 1000watapata mafunzo hayo ambayo yatakuwa kwa muda wa wiki mbili na zaidi.
Mrakibu Ngowi alisema kuwa jeshi lao limeamua kuanzisha mafunzo hayo ni baada ya kuona waendesha pikipiki ni moja ya sehemu kubwa katika jamii na wengi wanakufa kwa sababu ya kutokujua sheria za barabarani.
"Tunaimani tukiwapatia mafunzo hayo wanaweza pia kufichua maovu mengi ambayo wanayoyapata na pia wataelimika kwa kujua alama za barabarani na jinsi ya kuendesha pikipiki"alisema Mrakibu Ngowi.
Aliongeza kuwa wahalifu wengi hujifanya wao ni dereva wa pikipiki na hata wengine kutumia pikipiki hizo kwa ajili ya kufanyia ualifu wao.
Hivyo ni vyema katika kituo chochote cha pikipiki wakimuona mtu ambaye hawamuelewi watoe taarifa upesi kwa jeshi la polisi ili hatua za kisheria zifatwe kwani hiyo itakuwa ni njia mojawapo ya kupunguza ualifu unaotokea
Pia alisema baada ya kupata mafunzo hayo watakuwa wameongeza polisi jamii kwa jamii kwa kuwa wanaimani kuwa wao wanajua mambo mengi ya mitaani ikiwemo kuwafichua waarifu.
Alisema kuwa kwa sasa jeshi la polisi limeamua lisiwe linawakamata waendesha pikipiki kwani wameona kuwa wengi wao hawana elimu ya kutosha juu ya sheria za barabarani.
"Ndio maana tunataka kuwapatia kwanza elimu na si kuwakamata kama ilivyo"alisema Mrakibu Ngowi.
Vilevile, alisema kuwa wanataka waendesha pikipiki wawe sehemu ya jamii na anaimani wakishirikiana jeshi hilo ajali na ualifu vitapungua.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment