07 September 2012
Airtel yamtangaza AY kuwa Balozi wake mpya
KAMPUNI ya simu za mkononi ya Airtel leo imemtangaza Ambwene Yessayah 'AY' kuwa Balozi wake mpya kwa mwaka 2012-2013 , ikiwa ni utaratibu iliyojiwekea katika kushirikiana na wasanii nchini ili kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.
AY ni msanii mahiri nchini kwenye muziki wa kizazi kipya aliyejipatia heshima na kuvuta hisia za wapenda burudani wengi pale anapokuwa jukwaani, AY alijulikana zaidi baada ya kuachia albumu yake ya kwanza iliyobeba wimbo mkali wa ‘Raha kamili” na kufanya apendwe zaidi kitaifa na kimataifa kuanzia mwaka 2001
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meneja Uhusiano wa Airtel Jackson Mmbando alisema wameingia makubaliano na AY lengo likiwa ni kuendeleza utaratibu wa kampuni hiyo kuwa karibu na wasanii.
“Airtel tumeingia makubaliano na msanii AY kuwa Balozi wetu wa mwaka huu, lengo letu ni kuendelea kuwa karibu zaidi na wasanii wetu nchini na pia kufanya nao shughuli za kijamii ili kufaidisha taifa letu kwa kuwa wasanii wetu ni mahiri zaidi na wote tunafahamu AY ni msanii mkongwe na anayejituma, hivyo tunaamini ushirikiano huu utaweza kutimiza malengo yetu ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa pamoja ili kuhudumia jamii kupitia miradi mbalimbali ya jamii inayoendeshwa na Airtel pamoja na kuiwakilisha Airtel kwa kuwa Balozi mzuri,” alisema
Alisema AY ni msanii mwenye umahiri wa hali ya juu pale anapokuwa jukwaani, AY ameshafanikiwa kufanya matamasha ya kimataifa huko USA, UK, Spain, Dubai, Burundi, Rwanda, Ethiopoa, Malysia, India, Russia, Afrika ya kusini, Kenya na Uganda ikiwa ni pamoja na kufanya nyimbo nyingi na wasanii wengi wa kitaifa na kimataifa
Wasanii waliowahi kufanya nyimbo na AY ni pamoja na Chameleon, Ngoni (Uganda) , Amani, Nameless, Jua Cali (Kenya), P.Square, J.Martins (Nigeria) wengine ni msanii wa kimataifa Ms.Trinity, Sean Kingston anayewika Jamaica pamoja na Lil Romeo wa USA
Aliongeza kuwa AY ni msanii wa kwanza wa kiume nchini Tanzania kutunukiwa tuzo ya KORA mwaka 2005, na kupata pia tuzo ya MTV MAMAs ya 2009 pamoja na kutunikiwa France Awards mwaka 2010. Na hivi sasa amechaguliwa katika kuwania tuzo za Channel O katika vipengele vitatu; Video bora ya Africa, Video bora ya mwaka na mwanamuziki bora wa kiume wa mwaka.
"Kwa kushirikiana na Airtel nitakuwa nikifanya shughuli za kijamii, hususani katika kuchangia ukuaji wa Elimu nchini, pamoja na Airtel tutashirikisha vyombo na taasisi nyingine ikiwemo vyombo mbalimbali vya Habari ili kuweza kufanikisha yote hayo. Kwa Kushirikiana na Airtel tutaandaa maonesho mbalimbali ya burudani kwa ajili ya wateja wetu na hii itatangazwa hivi karibuni.
“Na kwa kuanza kama balozi wa Airtel napenda kuwaomba na kuwaimiza Watazania wenzangu kuweza kuchangia mradi ambao tumeshauanzisha wiki tatu zilizopita tukishirikiana na BAMVITA katika kuchangia vitabu kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum. Kampeni hii ya ushirika na Bamvita itaendeshwa kwa muda wa miezi mitatu, na Watanzania tunaweza kuchangia kwa kutuma neno “Vitabu” kwenda namba 15626 na kwakufanya hivyo kila SMS tutakayotuma utakuwa umechangia shilingi 200 itakayoingizwa yote katika mradi huu,” alisema AY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment