05 September 2012

Majaji na Mahakimu wakigoma, nani atatoa haki?



Na Mwandishi Wetu

HIVI karibuni, nilibahatika kuwa katika kikao fulani kilichofanyika jijini Dar es Salaam, kikiwahusisha pia Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta, Msajili wa Vyama vya Siasa Mstaafu, Jaji George Liundi na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Amer Manento.

Kwa idhini ya Mwenyekiti, niliwauliza majaji hao kama Rais ana uwezo wa kumtimua kazi jaji yeyote na wakati wowote.
Majaji wote walisema, majaji hata kama wametenda kosa la kuwalazimu kuwajibishwa kwa kuondolewa kazini, sio haki wala wajibu wa rais kutoa adhabu.

Kwamba inapotokea suala linalolazimu kutiliwa shaka majaji, inabidi kuundwa chombo maalumu cha majaji watatu toka nchi tatu za Jumuiya ya Madola mmoja akiwa Mtanzania (nchi ya jaji/majaji mhusika) na wawili, kutoka nchi za nje, hao kwa vigezo vya kitaaluma, huchunguza tuhuma na wanaporidhika kuwa jaji anayetuhumiwa ametenda kosa, basi hupendekeza adhabu na si vinginevyo.

Jaji Samatta akasema, “Utaona kwamba wakati hakimu au Jaji amekaa pale anaendesha hukumu, huwa hana mwajiri kabisa, yuko huru kufanya kazi yake ya kugawa haki za kisheria kwa haki. Hapo, hata kama kutakuwa na maelfu ya watu nje ya mahakama wanaandamana kushinikiza fulani (mtuhumiwa aachiwe) au wakishinikiza aadhibiwe, hilo haliihusu mahakama” wala halizuii haki kutolewa kwa anayestahili kwa mujibu wa sheria.

Akasema, “Mahakama inabaki palepale ikiwa huru kutenda haki za kisheria kwa pande zote bila hofu ya shinikizo la maandamano wala mwajiri au muhimili mwingine wa dola. Hivyo, siyo kweli kwamba wakati wowote Rais akipenda anamfukuza kazi Jaji; hapana. Majaji ni tofauti na mawaziri au wateuliwa wengine kama wakurugenzi, n.k”.

Kwa utangulizi huo, niseme wazi kwamba kamwe sikubaliani, wala siungi mkono harakati zinazoendeshwa za kumshinikiza Mheshimiwa Rais atengue uteuzi wa majaji. Hata hivyo mwenendo wa harakati hizo dhidi ya mahakama, umekosa adabu na mwelekeo wa kujenga na badala yake ni kubomoa hadhi na heshima ya mhimili wa mahakama.
 
Hata hivyo, kusitasita kwenu kuendesha kesi za watu walioamua kuishi maisha ya kiuchochezi unayaweka makundi mengine katika jamii katika hatari kubwa.

Ni vigumu kutabiri mnachotaka kitokee katika nchi, lakini mwenendo wenu dhidi ya kesi za wachochezi unatoa picha isiyoeleweka katika jamii.

Fikra yangu kuhusu hali hiyo, inanipeleka kuwaza kwamba labda na ninyi mko katika mgomo baridi, mmefikiwa upepo na kushawishiwa ili mgome kugawa haki ili jamii iamue kujigawia haki kama ipendavyo.

Lakini ikumbukwe kwamba, wakati mnatekeleza mgomo wenu, je mmewajulisha wadau wenu wa haki jinai nao waungane na ninyi?
Nimefikia hatua ya kuwaza hivyo, kutokana na mrorongo wa matukio ya kiuhaini yanayojitokeza nchini sasa.

Kwa mfano, wiki iliyopita Jeshi la Polisi limeandamwa na habari zinazolihusisha kusababisha kifo cha muuza magazeti mjini Morogoro wakati likizuia maandamano ya Chadema.

Lakini baada ya taarifa ya awali ya uchunguzi umma umeambiwa kwamba, kifo hicho hakikusababishwa na risasi wala bomu la machozi, sasa inadhaniwa huenda kuna mtu alitumia mwanya wa shughuli ya Polisi kutuliza ghasia na kurejesha utawala wa sheria akamfanyia marehemu alivyotaka.

Yamesemwa mengi kuhusu suala hili na tuhuma dhidi ya Polisi kiasi kwamba, wengine kupitia uhuru wa mawazo ninaouheshimu sana, tuhuma zote wameziweka juu ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema na Mkuu wa Operesheni wa Jeshi hilo, Kamishna wa Polisi (CP) Paul Chagonja wakisema wanalindwa na nani?

Wanaojenga hoja hiyo, ni kama vile wanasema kama wasingekuwa viongozi hao wa Polisi, mauaji kama hayo yasingetokea. Hili mimi naona linaongozwa na chuki binafsi dhidi ya viongozi hao wa Polisi, maana siamini kama hao ndio waliorusha kitu hicho kilichomuua muuzaji wa magazeti.

Nisingesema ni chuki binafsi, kama tuhuma kama hizo zingeelekezwa kwao kwamba walipaswa kuhakikisha wakuu wa Polisi wa wilaya au mikoa, wanatimiza wajibu wao wa kuwalinda watu wote (hata huyo muuza magazeti).

Nionavyo, lawama zilizorushwa kwa viongozi wakuu wa Polisi ni za wanaoangalia jamii ilipoangukia, badala ya kuangalia ilipojikwaa; na huku ndiko uitwa ni “kukataa ukweli” wa chanzo cha vurugu zinazowafikisha huko, wala si IGP Mwema wala CP Chagonja, bali ni mfumo na kasumba ya ulibukeni wa kulalamika iliyojengeka katika jamii yetu.

Kwamba baadhi ya wanasiasa “wameiroga” jamii na kuiambukiza ugonjwa hatari wa kuamini kuwa kila jambo lazima lishughulikiwe kwa kulalamika, migomo, maandamano na vurugu; tena kila siku na wakati wowote.

Jamii inalishwa sumu ya ugonjwa wa kuonewa huruma, hata pale anayetaka huruma anapofanya makosa na kuyarudia kwa makusudi, lakini akitaka ushurutishaji wa utii wa sheria za nchi umwonee huruma!

Ndiyo sababu nasisitiza umuhimu wa mahakama kuacha kuwa watazamaji, ila wachukuaji wa hatua kulingana na sheria za nchi. Ububu wa mahakama zetu katika kutekeleza majukumu yake unaweza kushusha ari ya vyombo vingine vya dola dhidi ya uhalifu huu mpya, ambao kimsingi ni hatari kwa sababu unaweza kusababisha mauaji ya haraiki.

Ninatambua na kuheshimu haki ya kuandamana au kugoma kwa amani, hususan katika mazingira ya sasa ya mfumo wa siasa za vyama vingi nchini, ambapo vyama vyote vinastahili haki sawa sambamba na wajibu wa kuimarisha amani na usalama kwa kutii amri na maelekezo ya vyombo vya dola bila shuruti.

Ikumbukwe kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye upungufu mkubwa wa askari Polisi usioenda sambamba na uwiano wa mahitaji ya idadi ya watu.

Hivyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu kukubali kukitumia kidogo kilichopo kwa utaratibu badala ya kundi moja dogo kutaka wao tu ndio wanufaike na huduma ya Polisi na kusahau maslahi ya walio wengi.

Hii pia inatokana na ukweli kuwa, Polisi wana taalauma, nyenzo na vyanzo vya kubaini viashiria mbalimbali vya uvunjifu wa sheria na amri halali. Pia ni wajibu wao kukabiliana navyo na si kuwachekea wanaovunja sheria au kukaidi maelekezo.

Sio siri, Watanzania na hasa baadhi ya vyama na baadhi ya wanahabari, tumefanya kosa la kutengeneza jamii inayoabudu kulalamika na vurugu. Vilevile wengine wanaona ni fahari kuwasilisha malalamiko na kero zao, kwa gharama ya maisha ya wengine.

Watanzania sasa tunaugua na kuendekeza ugonjwa wa kupingana na taratibu, kanuni na sheria za nchi na ndiyo maana mara nyingi, tunashuhudia vitendo vya kujichukulia sheria mikononi. Ikumbukwe kwamba, kujichukulia sheria mkononi ni pamoja na kuamua kuandamana au kufanya mikutano ya hadhara wakati unajua kwamba nimekatazwa kufanya hivyo na waliopewa mamlaka hayo kwa mujibu wa sheria.
Jamii ya watu makini inahoji kwamba, hiki ni chama gani kisichotaka kusikiliza wengine wanasemaje, wala kujali mahitaji ya kiusalama kwa makundi mengine!

Hicho ndicho kinachoitwa katika maandiko matakatifu tabia mbaya ya kujipenda mwenyewe, kwa sababu tunahimizwa kuwapenda na kujali mahitaji ya wengine kwanza kabla ya kuangalia ya kwetu.


Nchi yetu inaendeshwa kwa utawala wa sheria, nitakuwa wa kwanza kuwalaumu Polisi endapo wataacha viongozi wa chama chochote cha siasa au kikundi cha watu wahamasishe watu kutotii sheria.

Wakati wote tukumbuke kwamba, kauli za kuhamashisha watu kuvunja sheria na kuchochea vijana kufanya vurugu hazipaswi kuvumiliwa na Polisi, kwa sababu huo ndio mwanzo wa kulitumbukiza taifa katika migogoro na vita.

Watanzania wanapaswa kuelimishwa umuhimu wa amani na usalama tulionao, kwa sababu ni nafuu kuzuia na kutuliza vurugu kuliko kuingia gharama ya kusaka amani.

Ndiyo maana ninasema, tukio kama hili lililotokea katika Mkoa wa Morogoro ni matokeo kupuuzia mambo madogo madogo na vyombo vya dola zikiwemo mahakama zetu na badala yake, hoja inahamishiwa katika matokeo ya uhalifu wao.

Kadhalika, tukio la Morogoro ni pato la Mahakama zetu kuchelewa kutoa hukumu za haki dhidi ya wachochezi, ili kila upande upate haki stahiki maana umma umechoshwa kusikia taarifa za majeruhi na vifo vinavyotokana na vurugu za ovyo ovyo zinazotokana na uchochezi wa kisiasa.

Inashangaza hata matukio kama hayo yanapotokea, viongozi wa harakati hizo wa kisiasa wanaachwa na badala yake, eti Serikali inaunda tume kuchunguza. Ndiyo maana ninasema, Watanzania tunafanya kosa kubwa kuangalia na kushughulikia tunapoangukia, na kupaacha tulipojikwaa.

Ndiyo maana ninaiuliza Mahakama kwamba, inasubiri nini kitokee ili itoe hukumu za haki na adhabu kwa wanaovuruga amani na usalama wa Tanzania? Je, mpaka wananchi wasiopenda vurugu nao watoke kuandamana ndipo muone umuhimu wa kutoa hukumu?

Kwamba anayetaka kuchoma nyumba ya mtu achome? Anayetaka kuandamana usiku aandamane iwe ruksa? Vibaka wafanye watakavyo, majambazi wafanye watakavyo, majambazi waingie mitaani watakavyo, wanasiasa wafanye watakavyo; kila mmoja kadiri ya matashi yake, hata wachawi wapande nyungo zao mchana!

Hii itakuwa ni demokrasia au uhuru na haki gani hizo zinazohatarisha haki, amani, na usalama wa wananchi wengine?

Hata hivyo, kuonyesha dalili za kuwachokoza askari kwa makusudi ni kutolitendea haki Jeshi ambalo watumishi wake wanalinda mabenki ambayo wananchi wanakwenda kuweka na kuchukua maelfu, malaki na mamilioni ya pesa huku walinzi hao wakati mwingine wakiwa hawajui kama familia zao zitapata walau uji wa muhogo usio na chachu.

Huko ni kuwachokoza na kuwapa kipindi kigumu walinzi wetu, wanaolala nje wakinyeeshewa mvua, waking’atwa na mbu na kupigwa baridi ndani ya giza linalovunjiwa ukimya wake na kelele za wadudu, vyura na mbwa walioonja harufu ya tishio la uhalifu, huku sisi (na wachochezi) tukiwa ndani ya nyumba zetu tukijadiliana na waume au wake/wachumba zetu  mintarafu maendeleo au ongezeko la idadi ya watu katika familia zetu. Ndiyo sababu nasisitiza kwamba, mahakama ziache mgomo ziendeshe kwa haraka kesi za wachochezi.

No comments:

Post a Comment