02 August 2012

Zitto: Nipo tayari kuchunguzwa *Adai tuhuma dhidi yake ni shinikizo la kisiasa


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema tuhuma za rushwa ambazo zinaelekezwa kwake ni shinikizo la kisiasa na kuvitaka vyombo vya dola, chama chake, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kuzifanya uchunguzi wa kina ili kuthibitisha madai hayo.

Bw. Kabwe aliyasema hayo mjini Dodoma jana alipokutana na waandishi wa habari ili kuzungumzia tuhuma hizo na kuongeza kuwa, huo ni uzushi kama mwingine wowote uliosambazwa kimkakati na yupo tayari kuwajibika kama atakutwa na hatia.

Alisema dhamana yake katika nafasi aliyonayo ni kubwa ambapo  taswira yake imeakisi njozi na matumaini ya wananchi wa jimbo lake, wananchi wanyonge na vijana wote nchini bila kujali itikadi zao kisiasa, jinsia, makabila pamoja na rika zao.

Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo tuhuma za rushwa ambazo zimeelekezwa kwake ni hisia potofu zilizopandikizwa na watu wasiopenda kuona jinsi alivyoweza kuwaunganisha Watanzania wasio na sauti dhidi ya vitendo vya hujuma kwa Taifa.

“Kwa kujiamini kabisa, naunga mkono suala la tuhuma za rushwa zinazotajwa kwangu zifanyiwe uchunguzwe wa kina na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, chama changu ili kujiridhishe pamoja na vyombo vya dola ili kupata ukweli.

“Nipo tayari kutoa ushirikiano kama nitahitajika kufanya hivyo pia nitawajibika kama nitakutwa nma hatia yoyote, kimsingi mimi nimesimamia kidete maadili ya uongozi bora katika maisha yangu yote ya siasa na sitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa hapa nchini mbali ya kuwepo mikakati ya kunidhoofisha,” alisema.

Bw. Kabwe alisema, amekuwa mbunge katika vipindi viwili tofauti ambapo hivi sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).

Kwa miaka saba sasa, kamati hiyo inasimamia mashirika 259 ya Umma si Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), pekee lakini upo mkakati wa kumuunganisha na baadhi ya wabunge ambao wanatuhumiwa kupokea rushwa.

Alisema mkakati huo unatekelezwa kwa njia mbalimbali kwani wapo baadhi ya watendaji serikalini ambao wamekuwa wakieneza na kutoa taswira kwamba, baadhi ya kauli zake anazotoa bungeni zinatokana na ushawishi wa rushwa.

“Zipo taarifa ambazo zimeandikwa katika kurasa za mbele za baadhi ya vyombo vya habari zikidai “Zitto kitanzini’’ au “Zitto sawa na popo nundu”, zikiashiria mimi ni mla rushwa.

“Waandishi wa habari na jamii, wamefikia kuaminishwa habari hizi kiasi cha wengine kuuliza kwa nini Zitto hakutajwa katika orodha iliyotolewa na Bw. Tundu Lissu,” alisema Bw. Kabwe na kuongeza kuwa, ni bora atoe ufafanuzi wa kinachoelezwa yeye ni mshiriki wa masuala ya rushwa hasa katika sekta ya Nishati na Madini

Alisema baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, chini ya Uenyekiti wa Meja Jenerali mstaafu, Robert  Mboma, kutangaza kumsimamisha kazi Mhandisi William Mhando ili kupisha uchunguzi wa baadhi ya POAC, ilimwandikia barua Spika wa Bunge Bi. Anne Makinda kumuomba aridhie uamuzi huo.

“Dhamira ya kamati yetu ni kuwaita Bodi ya TANESCO, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), ili kujiridhisha na tuhuma zinazotajwa kufanyiwa uchunguzi wa kina.

“POAC ilimuomba Bi. Makinda kuwaita wahusika kwani kulikuwa na tetesi kuwa, kusimamishwa Mhandisi Mhando siku chache kabla ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kulikuwa na lengo la kufunika ’madudu’ makubwa zaidi kwa kulichagiza Bunge,” alisema.

Bw. Kabwe alisema, yeye binafsi anaona mkakati huo umefanikiwa sana ambapo kamati ya POAC kutaka kujiridhisha ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake yaliyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge kwani TANESCO ni kati ya mashirika ambayo yanawajibika kwo kwa hesabu zake na ufanisi.

Alisema kitendo kilichofanywa na kamati yake, kimetafsiriwa kwa makusudi na baadhi ya watu kuwa ni ishara ya wajumbe wake pamoja na yeye kuwa na masilahi binafsi na TANESCO hasa kwa Mhandisi Mhando.

Aliongeza kuwa, akiwa mjini Dodoma mwandishi mmoja wa habari alimfuata na kumwambia wamekutana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Bw. Eliachim Maswi na kuambiwa yeye amepewa rushwa bila kutaja na na nani, kiasi gani na kwa lengo gani.

“Nilijaribu kumtafuta kwa simu Prof. Muhongo na Bw. Maswi ili wanipe ufafanuzi juu ya mimi na Kamati ya POAC kuhusishwa na tuhuma hizi bila mafanikio hali ambayo iliniondolea mashaka juu ya ushiriki wao kueneza au kuthibitisha uvumi huo.

“Binafsi sijawahi kuwa na mawasiliano ya aina yeyote na uongozi wa TANESCO na kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndio imezichukua za kutaka kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika.

“Mchango wa Kamati hii katika Bunge na ustawi wa Mashirika ya Umma haujawahi kutiliwa shaka, tumeokoa upotevu mkubwa wa mali na fedha za umma kutokana na umakini wake,” ALISEMA.

Alisema zipo hoja pandikizi za kutaka POAC ivunjwe hasa zikimlenga yeye kwani anafahamu kiu ya wasioitakia mema Tanzania kutokana na umakini walionao wajumbe wa kamati.

Aliongeza kuwa, kwa maoni yake POAC isihusishwe na tuhuma hizo kwa vyovyote na yuko tayari kuhukumiwa yeye kama yeye badala ya kuhusisha wajumbe wengine ambao hawatajwi mahala popote katika tuhuma mbaaya katika historia ya Bunge nchini.

“Nitakuwa tayari kuinusuru POAC na masilahi ya Taifa kwa kujiuzulu Uenyekiti kama itathibitika pasipo shaka kuwa amehongwa, kamati hii ni muhimu kuliko mimi.

“Nafahamu kuwa, kuna wanasiasa hasa wa upinzani ambao wanautaka Uenyekiti wa POAC na kufanya kila njia ili kuidhoofisha lakini hawajui kama anaepanga wajumbe wa Kamati ni Spika wa Bunge,” alisema Bw. Kabwe.

Bw. Kabwe alisema, hivi sasa kumejengeka tabia ya kuwamaliza wanasiasa wenye kudai uwajibikaji na uzalendo na kuanzishwa kiwanda kwenye medani ya siasa cha kuzalisha majungu na fitna zenye lengo la kuwachonganisha wanasiasa na wananchi wakitumia vyombo vya habari na nguvu ya fedha.

“Naamini mbinu hizi chafu, kama nyingine nyingi zilizojaribiwa kwangu huko nyuma nazo zitashindwa, sitasalimu amri mbele
ya dhamira ovu hata nitakapobaki peke yangu katika mapambano ili kulinda na kutetea rasilimali za Taifa zinufaishe Watanzania wote.

“Daima nitaongozwa na busara ya Hayati Shabaan Robert isemayo, 'Msema kweli huchukiwa na marafiki zake, nitakapofikwa na ajali hiyo, sitaona wivu juu ya wale wawezao kudumu na marafiki zao siku zote, siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo, nikajitenga na furaha ya kweli itakayotokea pale uwongo utakapojitenga,” alisema.

4 comments:

  1. Kweli Tanzania ndipo tulikofika sasa?

    ReplyDelete
  2. NGOMA ikivuma sana mara upasuka.bw.mdogo ndani ya cdm hutakiwi na ccm hutakiwi dunia itakufunza....

    ReplyDelete
  3. usiogope ZITO endelea tutetee wananchi tumechoshwa na uongozi wa sasa kila mtu anataka kula

    ReplyDelete
  4. zitto, your days are over. waulize watu wa kigoma wanaojua ukweli na halisia yako. pole mwanangu

    ReplyDelete