16 August 2012

Zitto ataka mjadala wa rada nchini uendelee



Na Agnes Mwaijega

WAZIRI Kivuli wa Fedha na Msemaji wa Kambi ya Upinzani bungeni, Bw. Zitto Kabwe, amesema kurejeshwa kwa chenji ya rada nchini hakuwezi kumaliza mjadala uliopo bali Serikali inapaswa kueleza hasara iliyosababishwa na ufisadi huo.


Taarifa aliyoitoa Dar es Salaam jana kwa vyombo vya habari, ilisema Serikali iwajibike kuueleza umma hatua stahiki za kisheria ambazo wamepanga kuzichukua dhidi ya watu waliohusika kuliingizia Taifa hasara kubwa.

Alisema chenji hiyo ni nusu ya ukweli kuhusu suala hilo kwani Serikali ilikopa dola za Marekani milioni 40 kutoka Benki ya Barclays ya Uingereza ili kununulia rada.

“Kambi ya upinzani inataka kujua kama mkopo huu umelipwa wote  na kiasi kilicholipwa, tunaitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), kufanya uchunguzi wa kina kuhusu manunuzi ya mafuta ya kuzalisha umeme ambayo hutumia sh. bilioni 42 za Serikali kila mwezi,” alisema.

Aliongeza kuwa, Wizara ya Fedha ambayo ndio Wizara mama ya PPRA, inapaswa kupeleka taarifa ya uchunguzi utakaofanywa na mamlaka hiyo kuhusu manunuzi ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya kuendeshea mitambo ya umeme bungeni.

“PPRA haipaswi kufumbia macho manunuzi yanayotafuna fedha nyingi za kigeni, manunuzi ya mafuta yamejaa mizengwe ya ufisadi licha ya upinzani kumtaka Spika aunde timu ya kufanya uchunguzi kwani pamoja na Kamati ya Bunge kutaka uchunguzi ufanyike katika manunuzi haya hakuna hatua inayochukuliwa,” alisema.

Alisema mpango wa manunuzi ya mafuta ambayo hutumika kuendeshea mitambo ya umeme, inaligharimu Taifa fedha nyingi kwani takwimu zinaonesha kuwa, Serikali inapaswa kutumia zaidi ya sh. bilioni 42 kila mwezi kuendeshea mitambo ya umeme wa dharura.

Bw. Kabwe alisisitiza kuwa, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT),ihakikishe akiba ya fedha za kigeni nchini inakuwa imara muda wote.

Aliongeza kuwa, fedha wanazolipwa watumishi hewa kwa muda mrefu ni nyingi hivyo zitumike kulipia madai ya walimu na madaktari.

Alisema Serikali imeshindwa kutimiza matakwa ya wafanyakazi kwenye sekta ya afya na elimu kwa madai ya ukosefu wa fedha ni wakati wahusika wanashuhudia kila mwaka sh. bilioni 70 zikiteketea kwa kulipa watumishi hewa.

“Kwanini Serikali inakosa fedha za kulipa madai ya walimu na inapata wapi fedha za kulipa watumishi hewa, inakosa vipi fedha za kuwalipa madaktari na manesi,” alihoji Bw. Kabwe.


No comments:

Post a Comment