16 August 2012

Balozi Kagasheki akanusha uvumi wa kuwahamisha wamasai 48,000


Na Mwandishi Wetu

WIZARA ya Maliasili na Utalii, imekanusha uvumi uliotolewa na shirika moja kupitia mtandao wake wa AVAAZ.org kuwa wamasai 48,000 wamehamishwa katika eneo la Serengeti, mkoani Mara.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana kwa vyombo vya habari na  Waziri wa Wizara hiyo, Balozi Khamis Kagasheki, imesema mtandao huo unadai eneo hilo limetolewa kwa Wafalme kutoka Mashariki ya Kati ili walitumie kwa uwindaji wa Simba na Chui.


Alisema mtandao huo umewataka watu kutoka mataifa yote duniani kujiorodhesha na kufikia 150,000 ili kumshinikiza Rais wa Jakaya Kikwete asisaini mkataba ambao umelenga kuwahamisha wamasai hao jambo ambalo halina ukweli wowote.

“Uvumi huu hauna ukweli wowote, kwanza hatua kama hii haiwezi kuchukuliwa na Serikali ya katika Hifadhi ya Serengeti kwani hakuna watu waishio ndani ya eneo la hifadhi.

“Kitendo hiki hakijapangwa kufanyika katika Wilaya ya Serengeti ambayo pia haina idadi ya wamasai wanaofikia 48,000, pia ndani ya hifadhi hii hakuna eneo lolote ambalo limetengwa kwa ajili ya Wafalme wa Mashariki ya Kati,” alisema.

Balozi Kagasheki aliongeza kuwa, Rais Kikwete hausiki kabisa na ugawaji vitalu vya uwindaji katika eneo lolote nchini bali kazi hiyo ni ya Wizara yao ambayo pia haijafanya hivyo katika eneo tajwa.

Aliwataka watu ambao wameoroshesha majina yao na wanaotarajia kufanya hivyo kupuuza umuvi huo kwani wamepotoshwa hivyo hawapaswi kusaini ili kubariki kitu wasichokujua wala hakipo.

No comments:

Post a Comment