27 August 2012

Yanga we acha tu Kigali *Yaichapa Polisi 2-1 *Simba anguruma Arusha


Na Zahoro Mlanzi

MABINGWA WA Kombe la Kagame, timu ya Yanga, imeendeleza wimbi la ushindi katika kambi iliyoweka jijini Kigali baada ya kuichapa Polisi Force ya jini humo kwa mabao 2-1 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa kwenye Uwanjwa Stade de Kigali.


Mechi hiyo ni yapili kwa Yanga ikiwa nchini humo ambapo siku chache zilizopita, iliifunga Rayon Sports mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa  Amahoro nchini humo.

Katika mechi hiyo, mabao ya Yanga, yalifungwa na mshambuliaji wa kimataifa kutoka Uganda, Hamis Kiiza na la pili lilifungwa na Simon Msuva.

Akizungumza kwa simu muda mfupi baada ya kumalizika kwa mechi hiyo jana, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya timu ya Yanga, Abdallah Bin Kleb alisema mechi ilikuwa na ushindani tofauti na ile ya kwanza dhidi ya Rayon.

Polisi ilianza kupata bao katika kipindi cha kwanza ambalo lilidumu mpaka dakika 45 za kwanza zikimalizika.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Yanga ilicheza kwa kujituma zaidi ambapo beki wa kushoto, Stephano Mwasika aliisawazishia timu yake bao.

Yanga iliendelea kuliandama lango la Polisi na dakika chache kabla ya kipyenga cha mwisho kupulizwa beki, Nadir Haroub 'Canavaro' aliifungia timu yake bao la ushindi.

Aliongeza timu hiyo inatarajiwa kutua jijini Dar es Salaam leo mchana na kuwaomba mashabiki wao kujitokeza kwa wingi kuja kumpokea beki wao mpya, Mbuyu Twite.

Katika hatua nyingine, gazeti la Sunday Times la nchini humo, lilieleza kwamba, Kocha wa Police, Goran Kopunovic aliutumia mchezo huo kwa ajili ya kuwapima wachezaji wake wapya, Yussuf Ndayishimiye na Innocent Habyariamana ambao wamesajiliwa kutoka Kiyovu SC na AS Kigali.

Police imeondokewa na washambuliaji wake, Laudit Mavugo na Meddie Kagere ambao wamekwenda kucheza soka la kulipwa katika timu za Afrika Kaskazini za Esperance na JS Kablyie pamoja na mabeki, Deo Othieno na Gilbert Kaze ambao wameachwa kutokana na kubanwa na kanuni mpya za soka nchini humo kuwa na wachezaji wachache wa kigeni.

Wakati huohuo, Mwandishi Wetu kutoka Arusha, anaripoti kuwa, mabingwa wa Ligi Kuu Bara, timu ya Simba, imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mathare United ya Kenya katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini humo.

Bao la Simba lilifungwa na Daniel Akuffo na la kusawazisha lilitokana na beki, Juma Nyosso kujifunga katika harakati za kuokoa hatari langoni mwake.

Kiungo Kigi Makasi aliyesajiliwa kutoka Yanga, aliifungia timu yake bao la ushindi na kuifanya timu hiyo itoke kifua mbele katika mchezo huo.

No comments:

Post a Comment