21 August 2012
Watakiwa kutunza miundombinu ya umeme
Na Eliasa Ally, Iringa
MKUU wa Shule ya Sekondari ya Kiwere, iliyopo Wilaya ya Iringa Vijijini, Bw. Ally Jenga, amewataka wanafunzi wanaosoma shule za kata, kutunza miundombinu ya umeme wa jua iliyowekwa kwa gharama za Serikali ili kuinua kiwango cha elimu nchini.
Bw. Jenga aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na gazeti hili juu ya umeme wa jua uliowekwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) shuleni hapo.
Alisema awali wanafunzi wa shule hiyo walikuwa na utamduni wa kuharibu mifumo ya nyaya za umeme na kusababisha wakose mwanga utawawezesha kujisomea baada ya muda wa masomo.
“Baada ya kufuatilia tatizo hili, wanafunzi walirudisha baadhi ya vifaa vya umeme kwa siri ambavyo tulivichukua, kuanza kufanya ukarabati upya na kuweka umeme wa jua.
“Hivi sasa tunatumia umeme huu ofisini, mabwenini na madarasani hivyo kuwawezesha wanafunzi kupata mwanga wa kutosha ambao tunaamini utasaidia kuinua kiwango cha elimu kwa wanafunzi,” alisema Bw. Jenga.
Aliongeza kuwa, TASAF imeweka mfumo huo wa umeme mwaka 2011 lakini baada ya muda mfupi, wanafunzi walianza kuiba betri, nyaya zake pamoja na vifaa vingine hivyo kusababisha wakose umeme miezi miwili.
Alisema umeme huo umewekwa katika madarasa saba, ofisi 13 za utawala na mabweni mawili.
Kwa upande wake, Mratibu wa TASAF wilayani hapa, Bw. Christopher Kajange, dhamira yao ni kuhakikisha shule zote nchini ambazo hazijapitiwa na umeme wa gridi ya Taifa, zinanufaika kwa kuwekewa umeme huo.
Aliwataka walimu, wanafunzi na viongozi mbalimbali wa kata ambazo sekondari zao zimewekewa umeme huo, kulinda miundombinu yake ili iweze kudumu muda mrefu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment