21 August 2012

Wanaotishia kususia sensa watakwamisha maendeleo


Na Salma Mrisho, Geita

MKUU wa Wilaya ya Chato, mkoani Geita, Bw. Rodrick Mpogolo, amesema baadhi ya viongozi wanaotishia kususia sensa, hawaitakii mema nchi Tanzania na kutaka kukwamisha maendeleo.

Bw. Mpogolo aliyasema hayo jana wakati akizungumza na madiwani ili kuwataka waongeze nguvu ya kuhamasisha wananchi kushiriki Sensa ya Watu na Makazi iliyopangwa kuanza usiku wa kuamkia Agosti 26 mwaka huu.


Alisema kitendo cha Wenyeviti wa vitongoji na vijiji kutaka kususia sensa, kitakwamisha dhamira ya Serikali kuweka mikakati ya maendeleo kwa wananchi wake.

“Kazi ya viongozi pamoja na mambo mengine ni kuhamasisha wananchi waone umuhimu wa jambo hili sasa kama itatokea na wao wanasusa, watakwamisha mpango huu na kuwanyima wananchi haki ya kuhesabiwa,” alisema Bw. Mpogolo.

Mratibu wa Sensa mkoani hapa, Erasmus Rugarabamu, alisema inasikitika kuona kuna suala hilo linachukuliwa kwa dhana tofauti na  baadhi ya viongozi wakati dhamira yake ni kuchochea maendeleo.

Alisema malalamiko ya Wenyeviti wa vitongoji na vijiji kuwa hawakushirikishwa ameyapokea hivyo anasubiri maagizo kutoka serikalini ili aweze kuyafanyia kazi.

No comments:

Post a Comment