29 August 2012
Washtakiwa wamkataa Hakimu
Na Rehema Mohamed
WASHTAKIWA wa kesi ya unyang'anyi wa kutumiwa siraha, jana wamemkataa Hakimu Waliyarwande Lema, anayesikiliza kesi hiyo kwa madai ya kutokuwa na imani naye.
Kesi hiyo ililetwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa ajili ya kusikilizwa ambapo washtakiwa hao ni Bw. James Warioba, Bw. Abdulkarim Hussein na Bw. Seif Lusonzo.
Kwa nyakati tofauti, washtakiwa hao waliomba hakimu huyo ajitoe kusikiliza kesi yao wakidai hawana imani naye hivyo arejeshe jalada hilo kwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo ili liweze kupangiwa hakimu mwingine.
Hata hivyo, washtakiwa wenzao Bw. Ally Mdege na Bw. Benjamin Macklin, walipinga maombi ya washtakiwa hao kuhusu jalada hilo kurudishwa kwa Hakimu Mfawidhi kwa sababu ya kuteseka mahabusu na kutaka kesi hiyo iendelea kusikilizwa.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh. milioni 15.5 nyumbani kwa Jaji John Mgeta wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Katika kesi hiyo, inadaiwa kabla ya kufanya wizi huo washtakiwa hao walimfunga kamba za miguu na mikono Jaji Mgeta na familia yake, kuwatishia na mapanga, visu na nondo.
Wakili wa Serikali, Bi. Beata Kitau, alidai kuwa Januari 18 mwaka huu, huko Ununio Tegeta, Dar es Salaam, washtakiwa walikula njama ya kutenda kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment