29 August 2012

Polisi waua majambazi 4 Tabora


Na Frank Geofray, Jeshi la Polisi Tabora

JESHI la Polisi mkoani Tabora, limewaua majambazi wanne katika mapambano ya kurushiana risasi kati yao na polisi baada ya jaribio lao la kutaka kuvamia Congres Centre, kuzuiwa na jeshi hilo.


Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Antony Rutta, alisema tukio hilo lilitokea Agosti 25 mwaka huu, majira ya saa tisa mchana katika Kijiji cha Kaliua Magharibi, wilayani Kaliua.

Alisema majambazi hao walikuwa wamefunika sura zao kwa vitambaa ambapo eneo walilotaka kuvamia, hutumiwa na wafanyabiashara wengi kufanya biashara zao.

“Hawa majambazi walikuwa na bunduki aina ya Shot gun na baada ya kudhibitiwa, polisi waliipata bunduki hii ikiwa na risasi 12 pamoja na maganda sita ambayo yaliokotwa eneo la tukio.

“Baada ya kutolewa vitambaa usoni, jambazi mmoja aliyeuwawa ametambulika kwa jina la Masud Haruna, mkazi wa Kijiji cha Imalamihayo, wilayani hapa na wengine hawajatambulika,” alisema.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi mkoani hapa limetoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

No comments:

Post a Comment