28 August 2012
Wanne wafariki katika matukio tofauti Dar
Neema Kalaliche na Mariam Said
WATU wanne wamefariki dunia katika matukio tofauti yaliyotokea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, alisema katika tukio la kwanza, mtoto Yaisi Mohamed (6), alikufa papo hapo baada ya kukanyagwa na gari wakati dereva wake akilirudisha nyumba bila kumuona.
Alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 10 jioni, eneo la Tandale Uzuri, ambapo dereva wa gari hilo lenye namba za usajili T 841 ALS, aina ya Toyota Dian, hajafahamika.
“Huyu dereva alikuwa kirudisha gari lake nyuma ili aweze kuingia barabarani, nyuma yake kulikuwa na mtoto ambaye alikuwa anacheza hivyo alimkanyaga na kumuua papo hapo,” alisema.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala na juhudi za kulitafuta gari na dereva wake zinaendelea baada ya kukimbia.
Katika tukio jingine, mwendesha pikipiki, Daudi Masenti (37), mkazi wa Kimara Mavurunza, maefariki dunia baada ya kugongwa na gari aina ya Fuso ambapo ajali hiyo ilitokea juzi saa mbili usiku katika barabara ya Kigogo Mwisho.
Alisema gari hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Bw. Julius Nchame (29), mkazi wa Kimara Mwisho ambaye alikuwa akitoke Kigogo polisi.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Mwananyamala ambapo Bw. Nchame anashikiliwa na jeshi hilo kwa upelelezi.
Wakati huo huo, mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaaka 7-8, amefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na gari ambalo halikuweza kufahamika mara moja.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marietha Komba, alisema tukio hilo lilitokea juzi katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi eneo la Jamatini wakati mtoto huyo ambaye alikuwa akiuza karanga, kugongwa na gari ambalo halikufahamika wala dereva wake.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na juhudi za kumtafua dereva na gari hilo zinaendelea.
Katika tukio jingine, mkazi wa Chanika Zabala, Alifa Khalidi (20), amefariki dunia baada ya kudumbukia kisimani wakati akichota maji.
Kamanda Komba alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 10 jioni, eneo la Chanika wakati marehemu akichota maji na inadaiwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifafa. Mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment