28 August 2012

'Wapuuzeni watu, vikundi vinavyotaka kukwamisha sensa'


Tumaini Maduhu na Andrew Ignas

MKUU wa Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, Bi. Regina Mgema, amewataka wananchi wilayani humo kuwa makini na kuwapuuza watu au vikundi vinavyoshawishi wasishiriki Sensa ya Watu na Makazi ili Serikali ishindwe kupanga mikakati ya maendeleo.

Alisema sensa ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya nchi na kupitia mchakato huo, Serikali itaweza kujua idadi kamili ya watu wake pamoja na changamoto walizonazo ili ziweze kufanyiwa kazi.

Bi. Mgema aliyasema hayo jana wakati akizungumza na makarani wa sensa wilayani hapa pamoja na kusikiliza matatizo ambayo wanayapata wanapotekeleza kazi waliyopewa na Serikali.

Aliongeza kuwa, mwananchi yeyote ambaye atakataa kuhesabiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni, atachukuliwa hatua.

Katika hatua nyingine Bi. Mgema, alikiri kupokea malalamiko ya ucheleweshwaji vifaa vya sensa na kuwaomba makarani waendelee na kazi wakati tatizo hilo likishughulikiwa.

Ofisa Mtendaji wa Kata Kijichi, Bw. Basil David, alisema uandikishaji wananchi katika kata hiyo unaendelea vizuri na tayari watu wengi wamehesabiwa.

“Viongozi tunasimamia vizuri kazi hii kwa kutembelea maeneo mbalimbali ya kata zetu ili kuhakikisha watu wanahesabiwa pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili makarani,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Meya Manispaa hiyo, Bw. Noel Kipungule, alisema sensa ilipaswa kuwashirikisha viongozi wa Serikali za Mitaa na wajumbe wa mashina kwa sababu wao ndio wanawafahamu wananchi.

No comments:

Post a Comment