27 August 2012

Waliomliza DC Nkasi kamwe wasichekewe, wachukuliwe hatua



MWISHONI mwa wiki, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa, Bw. Idd Kimanta, aliangua kilio kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani mjini Namanyere, baada ya kusikitishwa na utendaji mbovu wa Mkurugenzi pamoja na Wakuu wa Idara mbalimbali.


Bw. Kimanta alilazimika kuangua kilio baada ya madiwani kumlalamikia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bi. Saada Mwaruka, Mwenyekiti wa Halmashauri Bw. Peter Mizinga pamoja na Kaimu Mtunza Hazina, Manka Mlinda.

Watendaji hao wanadaiwa kushindwa kuwasilisha agenda ya ukaguzi wa mahesabu ya halmashauri hiyo kwa muda mrefu sasa tangu baraza hilo litoe agizo katika kikao cha Machi na Juni 2012.

Kutokana na hali hiyo, madiwani hao waliamua kuwatolea uvivu watendaji hao wa Wilaya baada ya kushindwa kujibu hoja 15 za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambazo zilisababisha Wilaya ipate hati ya mashaka.

Pamoja na Bw. Kimanta kutoa chozi akisikitikia vitendo ambavyo vimefanywa na watendaji hao, hakusita kusema ni kashfa kubwa kwa madiwani kutopelekewa taarifa za mahesabu.

Alisema kama wataendelea na msimamo wao, Wilaya hiyo itashindwa kupewa fedha kutoka serikalini jambo ambalo halitawatendea haki wananchi.

Sisi tunasema kuwa, watendaji wote waliomliza Bw. Kimanta kwa kuhusishwa na kiburi cha utendaji wa majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi, kamwe wasichekewe bali wachukuliwe hatua.

Ni wazi kuwa, changamoto nyingi zilizopo katika halmashauri mbalimbali nchini ni ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo unaofanywa na watendaji wasio waadilifu.

Hali hiyo inachangia umaskini mkubwa katika jamii na kukwamisha maendeleo ya sekta mbalimbali kijamii na kiuchumi.

Fedha nyingi za umma zinaishia mikono ya wajanja wachache ambao wanaishi maisha ya kifahali tofauti na kipato chao.

Inasikitisha kuona baadhi ya halmashauri, ubadhirifu wa fedha za maendeleo unafanyika kana kwamba hakuna wakaguzi na kusababisha majengo mengi sambamba na miradi mingine kutokidhi viwango vya ubora.

Umefika wakati wa watendaji wote waliopewa dhamana ya kusimamia sera za nchi, kutekeleza wajibu wao bila kushurutishwa na kukiuka taratibu za matumizi ya fedha kwani vitendo hivyo vinachangia watoe taarifa zinazohusu ukaguzi ambazo si sahihi.

Tunaamini msimamo wa madiwani hao utasaidia kuwepo uwazi na uwajibikaji kwa watendaji ili mwananchi ajue bajeti inatumikaje na kitu gani kinatakiwa kufanyika ili kumletea maendeleo kulingana na mapendekezo ya vipaumbele vilivyoombewa fedha.

No comments:

Post a Comment