27 August 2012

Serikali kuwafikishia huduma za simu wananchi-Dkt.Mgimwa


Na Eliasa Ally, Iringa

WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Dkt.William Mgimwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa amesema Serikali itahakikisha wananchi ambao hawafikiwi na mawasiliano ya simu za mkononi hususan katika maeneo ya vijijini inawajengea minara.

Alisema, tayari Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano imetengewa fedha za kukabiliana na hali hiyo.

Hayo aliyasema jana baada ya wakazi wa jimbo hilo katika vijiji ambavyo vinakabiliwa na ugumu wa kupata mawasiliano ya simu, kumuomba mbunge wao awasaidie kuziomba kampuni za simu kuwajengea minara ili kuwarahisishia mawasiliano wanayohitaji.

Vijiji vya Jimbo la Kalenga ambavyo havina mawasiliano ya simu ni pamoja na Ilalasimba, Magubike, Itagutwa, Kitapilimwa, Ikungwe, Ihomasa, Kata za Maboga, Kiponzero na Mgama ambapo wakazi wa vijiji hivyo walilalamikia kukosa mawasiliano ya simu kwa mbunge wao.

Dkt.Mgimwa alisema kuwa Serikali tayari imeviorodhesha vijiji visivyokuwa na mawasiliano ya simu nchi nzima, vikiwemo na vijiji hivyo vya Jimbo la Kalenga na kuongeza kuwa tayari serikali imetenga bajeti itakayowezesha kujengwa na minara ya mawasiliano katika maeneo hayo.

Aidha, aliwataka wananchi hao kuwa na subira wakati wizara husika ya mawasiliano ikilishughulikia suala la kero ya mawasiliano katika vijiji vyote na kuongeza kuwa katika dunia ya leo mawasiliano ni njia ya msingi ya kujulishana na kutaarifiana habari.

"Katika dunia ya leo unapozungumzia mawasiliano ya simu za mkononi, unaongelea suala nyeti, hivyo tayari Serikali imeona umuhimu wa sekta hiyo na vijiji vyote nchi nzima vimejumlishwa na kupatiwa bajeti ambayo itatosheleza kujenga minara na watu wote wafikiwe na mawasiliano ya simu za mkononi," alifafanua Dkt.Mgimwa.



No comments:

Post a Comment