17 August 2012

Waislamu endelezi matendo mema ya mwezi mtukufu;Sabouri




Na David John

MWEZI mtukufu wa Ramadhani kwa waislamu ni moja kati ya nguzo za uislamu ambapo waumini wa dini hiyo wanahitajika kufunga ikiwa ni moja wapo ya ibada ambayo ni wajibu kwa kila muislamu kuitekeleza.

Kuwepo kwa mifungo hiyo ni moja ya njia ya kujitakasa baada ya kuwa katika dhambi kwa muda mrefu, hivyo ili kujitakasa waumini hao wameuweka utaratibu wa kuwepo kwa mwezi mmoja katika kipindi chote cha mwaka mzima kumlilia mungu na kutubu makosa yao.

Toba ni kitu muhimu kwa wanadamu kwani wamekuwa watu wakumkosea Mwenyezi Mungu kila iitwapo leo hivyo lazima kutenga muda wakurudi kwake na kupiga magoti ili kuomba Toba ya kusamehewa Dhambi.

Ukuu na hali ya mwezi mtukufu wa Ramadhani si kwa sababu ya kufunga swaumu, bali utukufu na ukuu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kwa kutokana na Qur’ani tukufu.

Ni mwezi wa Imani, msamaha, mwezi ambao ndani yake kuna 'usiku' (Mmoja) ambao ni bora kuliko miezi 'Elfu moja' kama alivyosema Allah  katika Suuratul Qadr aya ya 3.

Mkurugenzi wa kituo cha Utamaduni cha Irani Bw.Morteza Sabouri, anasema kuwa kufunga ni moja ya agizo la Mungu hivyo lazima wanadamu hasa waislamu watumie siku 30 za kufunga kumalilia mungu dhambi zote ambazo zimetendwa katika kipindi cha mwaka mzima.

Anasema pamoja na kufunga lazima aonyeshe uhalisia wa kile anachokifanya na siyo vinginevyo, na siyo kujenga dhana na wajibu wa kufanya hivyo kwakua ni muislamu.

Anasema kama mtu anafunga ahakikishe anafunga kweli ikiwa pamoja na kufuata taratibu za sala kwa mujibu wa maelekezo ya kitabu tukufu cha Mwenyezi Mungu yaani QURAN.

Bw. Sabouri anasema kuwa changamoto zipo nyingi hasa katika kipindi hicho cha mfungo wa ramadhani hivyo kuna kila haja ya kuhakikisha waislamu wanapambana na changamoto hizo ili kupata kile wanachokihitaji kutoka kwa Mungu.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo anasema kuwa mwiislamu asisubiri toba mpaka mwezi huu bali iwe wajibu wake kila siku kuomba toba.

Bw, Sabouri anasema kuwa hakuna haja ya kujionyesha kuwa unafunga wakati matendo yako hayafanani na kile unachokiamini kwa wakati ule ni sawa na kujilia hukumu yako mwenyewe.

Anasema kuwa mwiislamu inatakiwa kutoa sehemu ya fungu lake kama sadaka hasa katika kipindi kama hiki cha mfungo wa ramadhani ili  kwenda sambamba na mfungo wako.

"Niwakati wakujitoa  mwenyewe na mali kwa ajili ya Mungu ili kujisogeza zaidi kwa mungu nakufanya mfungo wako kukubalika zaidi na Mungu"anasema Bw. Sabouri.

Anasema watanzania wamejaliwa amani na utulivu ndani ya nchi yao hivyo nifursa pekee ya kuweza kumtumikia Mungu kwakuwa nchi imekuwa tulivu na usalama zaidi.

Anasema mataifa mengine wanakosa hata muda wakuweza kufanya mambo ya mungu kutokana na kutawaliwa na vurugu  katika nchi hizo kitua ambacho kinapelekea wasipate hata muda wakumuabudu Mungu wao.

"Fursa hii inatakiwa kutumia vizuri kwani hata mwisho wa siku unaweza shindwa kujitetea kwasababu utakuwa hauna cha kusema," anasema.

Bw.Sabouri anasema kwa kutambua hilo kituo chake kipo mstari wa mbele katika kutoa mafundisho ili kufanya waislamu kukomaa zaidi kiimani na kuona kile wanachokifanya hawabahatishi.

Bw. Sabouri anaongeza kuwa msingi mkubwa wa kuweza kushikilia imani ya mtu lazima uwe mtu wa kusoma vitabu vya Mungu kila wakati na kutii kile unachoelekezwa kupitia vitabu hivyo.

Mmoja wa maofisa kituoni hapo Bw.Piran anasema iman ni jambo muhimu katika maisha ya mwanadamu kwani bila kuwepo kwa hali hiyo yanayofanyika duniani leo yangekuwa mara mbili.

Anasema binadamu wamekuwa wakifanya mambo ambayo ni chukizo kwa Mungu lakini kitu pekee kinachosaidia ni imani, hivyo kuna haja ya kushikilia imani hiyo ili mwisho wa siku iwe mkombozi katika maisha ya mwanadamu.

"Nawakumbusha waumini wezangu wa kiislamu fungeni kwa imani na thawabu yenu mtaipata siku hiyo," anasema Bw. Piran.

Anaongeza kuwa pia imani inafuata matendo hivyo bila shaka baada ya kumaliza mfungo waislamu mtaendelea kutenda mema daima, na siyo kurudia kufanya maovu.

"Inasikitisha sana pale unapomuona muumini mzuri wa kiislamu anafanya mambo tofauti na uislamu na unavyolelekeza halafu anajisifu kuwa yeye ni muumini wa kiislamu,"

"Kuweni watu wa tofauti na wenye mfano wa kuigwa hata ambaye siyo mwiislamu avutiwe na kile ambacho muumini huyo anakifanya kwa ajili ya utukufu wa mungu," anasema.

Anaongeza kuwa uislamu unaenda sambamba na kujali wengine na kuwa na moyo wa kujitoa katika kipindi chote cha maisha yako katika dunia.

Anatoa rai kwa viongozi wa dini hiyo kuwa watu wa kuelekeza bila kuchoka kwa waumini wao ili kuweza kutoa elimu ya nini Mtume anahitaji kutoka kwa waumini wake, na kukumbushia kile ambacho mtume alikuwa akifanya kwa ajili ya Mungu.

Anasema Irani mbali na kuwa na uchumi unaoridhisha lakini watu wake wana muamini sana Mungu na ndiyo maana wamekuwa mstari wa mbele kufanya yanayompendeza Mungu.

Bw. Sabouri anawatakia waislamu wote sikukuu njema na wasiache kumcha Mwenyezi Mungu na badala yake waendeleze mazuri yote waliyokuwa wakiyatenda wakati wa ramadhani

Anasema upendo ni kitu muhimu na Mungu amewataka waja wake kuweka upendo baina yao ili kufanya huduma yake kuwa nyepesi na yenye kibali mbele zake. Pia tufuate tuliyoyatenda katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.


No comments:

Post a Comment