21 August 2012
Misamaha ya kodi sasa itatazamwa upya-Pinda
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu, Bw.Mizengo Pinda, amesema ipo haja ya kulitazama upya suala la misamaha ya kodi ambayo inatolewa na Serikali kwa mashirika ya dini na taasisi za kijamii.
Alisema lengo ni kuhakikisha misamaha hiyo haiwaongezei gharama za malipo kwa mizigo yao kukaa bandarini muda mrefu.
Bw.Pinda aliyasema hayo mjini Dodoma juzi wakati akizungumza na wakazi wa mkoa huo ambao walihudhuria sherehe za miaka 10 ya Kijiji cha Matumaini, kinacholea watoto yatima kilichopo eneo la Kisasa nje kidogo ya mji huo.
“Serikali imekuwa ikitoa misamaha ya kodi lakini hatuna mfuko uliotengwa kwa ajili ya huduma kama hizi lakini bado tunamtaka Waziri wa Fedha akusanye pesa,” alisema Bw.Pinda.
Ufafanuzi huo wa Bw.Pinda ulitokana na risala ya uongozi wa kijiji hicho kuiomba Serikali ifikirie kuruhusu mizigo iliyoombewa misamaha ya kodi itolewe bandarini chini ya utaratibu maalumu wakati taratibu za kuandika hundi zikiendelea kwani uhakika wa kulipa kodi hiyo upo.
Katika risala yao, viongozi hao walimweleza Bw.Pinda adha wanazopata kwa kusubiri mizigo iliyoombewa msamaha wa kodi itoke bandarini kwa sababu huchukua muda mrefu hivyo malipo ya kutunza mizigo huongezeka siku hadi siku.
“Wakati tunasubiri hundi ziandikwe kutoka hazina kwenda Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na bandarini, malipo ya kuweka mizigo yanaongezeka,” walisema.
Walisema adha nyingine ni ucheleweshaji wa dawa na viini lishe kwa watoto wanaowahudumia ambao baadhi yao wanaishi na virusi vya UKIMWI.
Kutokana na hali hiyo, waliiomba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, iangalie uwezekano wa kukipatia kijiji hicho ruzuku kutokana na huduma wanazotoa kwa watoto hao na wakazi wa vijiji jirani.
Akitoa mahubiri katika ibada maalumu ya shukrani kwa kutimiza miaka 10 ya kijiji hicho, Askofu mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dodoma, Mhashamu Mathias Isuja, alisema jamii haina budi kuwalea watoto katika imani na maadili mema ili wajifunze kumpenda Mungu.
”Jamii imepewa jukumu la kulinda uhai wa mtoto na kuwalea ili wawe wacha Mungu na raia wema wa baadaye,” alisema.
Kijiji hicho kilianzishwa Agosti 17, 2002 kikiwa na watoto watatu na familia moja ambayo ilikuwa ikiwatunza watoto hao Hassan, Amani na Neema ambao walikuwepo katika maadhimisho hayo.
Hivi sasa kina watoto 163 wanaoishi kwenye familia 13 chini ya uangalizi wa baba na mama kwa kila nyumba na kati yao, 95 wako shule za msingi, 10 sekondari, wanane wanasoma kwenye vyuo vya ufundi na waliobakia wengine wako shule za awali.
Wakati huo huo, Bw.Pinda aliendesha harambee ya papo kwa papo na kukusanya sh. milioni 20, ambazo ni ahadi na fedha taslimu kwa ajili ya kukisaidia kijiji hicho.
Ahadi zilizotolewa ni magunia matano ya mahindi, kilo 100 za mchele, mafuta ya alizeti lita 20 na unga wa mahindi mifuko 50.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment