31 August 2012
Twite akata mzizi wa fitna *Atua Dar, atamba kufanya makubwa
Na Charles Lucas
HATIMAYE ile filamu ya beki mpya wa Yanga, Mbuyu Twite imemalizika jana baada ya kuwasili Dar es Salaam na kukata mzizi wa fitna.
Ujio wa beki huyo mzaliwa Congo DRC aliyesajiliwa kutoka APR ya Rwanda, ulizua utata baada ya uongozi wa Simba ambao ni watani wa jadi wa Yanga kudai kwamba akifika watamkamata kwa kuwa alichukua dola 30,000 kwa ajili ya kuichezea timu hiyo, lakini amewageuka.
Mchezaji huyo aliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) saa 10 jioni na kupata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki, wanachama na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo akiwemo Katibu Mkuu, Selestin Mwesiga.
Baada ya kutokeza nje ya jengo la uwanja wa ndege mashabiki hao waliripuka kwa shangwa na vigelele, huku wakimzonga kutaka kumuona na kusababisha tafrani hali iliyosababisha apitie mlango maalumu unaotumiwa na wageni rasmi (VIP).
Akizungumza na wandishi wa habari mchezaji huyo, ambaye amekamata kitita cha dola 50,000 alisema yeye amekuja nchini kikazi zaidi na atahakikisha kwa kushirikiana na wachezaji wenzake wanaipaisha Yanga.
"Mengi yanasemwa, lakini nipo hapa kwa ajili ya Yanga na nitafanyakazi kadri ya uwezo wangu ili kuitumikia timu yangu," alisema.
Mchezaji baada ya kutoka nje ya mlango wa uwanja alipanda gari dogo (Hiace) la klabu huku akisindikizwa na msafara mkubwa wa magari na pikipiki.
Mashabiki hao waliokuwa na bendera za timu hiyo walikuwa wakiimba nyimbo za kuikejeli viongozi wa Simba, ambao awali walitamba kumsajili Twite lakini wakapigwa chenga ya mwili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment