31 August 2012

CHANETA yafanikiwa kwa mara ya kwanza



Na Amina Athumani

CHAMA cha Netiboli Tanzania (CHANETA), kimesema kwa mara ya kwanza michuano ya Ligi Daraja la Kwanza imefanikiwa kukusanya timu nyingi zaidi, tangu kuanzishwa kwa chama hicho ikiwa ni pamoja na timu zote kulipa ada ya ushiriki.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa CHANETA, Rose Mkisi alisema hiyo ni dalili kubwa ya kukua kwa mchezo huo kwani katika miaka iliyopita mashindano hayo yamekuwa yakishirikisha timu zisizozidi 12.

Alisema kwa mwaka huu jumla ya klabu 19, zimefanikiwa kukamilisha taratibu zote za mashindano ikiwa ni pamoja na kulipa ada ya ushiriki, kufanya usajili kwa ufasaha nlakini kwa miaka ya nyuma timu nyingi ziliona ugumu kulipa ada.

"Hii haijawahi kutokea hata mwaka mmoja tukaendesha mashindano ya ligi na timu zikakamilisha taratibu zake kama mwaka huu, ambapo mbali na kukamilisha taratibu hizo pia idadi kubwa ya timu zimeongezeka katika ligi hiyo tofauti na miaka ilkiyopita," alisema.

Alisema hiyo pia imetokana na wao kama CHANETA, kusimamia kikamilifu kanuni za sheria za mashindano hayo tofauti na mashindano mengine yaliyopita, ambapo wamekuwa wakioneana huruma huku timu nyingine zikiruhusiwa kushiriki kwa mkopo.

Katibu huyo alisema kutokana na hali hiyo, kumeifanya CHANETA kuandaa taratibu za mashindano hayo bila kutetereka na ratiba kamili inatarajia kuanza Septemba 13 mwaka huu.

Alisema mechi zitaanza kuchezwa Septemba 14 mwaka huu, huku wakitarajia wachezaji waliopewa ruhusa kwa ajili ya kazi ya sensa kujiunga na timu zao kwa ajili ya mashindano hayo.

No comments:

Post a Comment