21 August 2012

Timu nne kikapu zaenda Uganda



Na Zahoro Mlanzi

TIMU nne za Tanzania za Kikapu zimeondoka leo kwenda Kampala, Uganda kushiriki mashindano ya kutafuta bingwa wa kikapu wa Kanda ya Tano ya Shirikisho la Mpira wa Kikapu Duniani (FIBA).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Phares Magessa, alisema timu hizo ni Savio kutoka Don Bosco ambao ndio Mabingwa wa Tanzania upande wa wanaume na washindi wa pili ABC, na kwa upande wa wanawake ni Jeshi Stars na Don Bosco Lioness.

Alisema kila timu imeondoka na wachezaji 12 na viongozi watatu ambapo Mkuu wa msafara ni Kamishna wa wanawake katika TBF, Meja Specioza Budodi ambapo baadaye viongozi wengine wa juu wa TBF watakwenda ambao ni Alexander Msoffe ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya FIBA Kanda ya 5.

"Mimi ndiye niliyeziaga timu hizo pale viwanja vya Chang'ombe leo (jana) asubuhi pia walikuwepo Kanali Busungu ambaye ni Mkurugenzi wa Michezo katika JWTZ, Katibu Mkuu wa TBF, Alexander Msoffe na Mkurugenzi wa kituo cha Don Bosco Father Swai," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Alisema kwa sasa bingwa mtetezi ni Urunani toka Burundi kwa upande wa wanaume na Kenya Ports Authority (KPA) toka Kenya ambao walichukua ubingwa katika mashindano yaliyofanyika Dar es Salaam mwaka jana.

Alisema mashindano hayo yanashirikisha timu mbili za wanaume na wanawake washindi wa juu kutoka katika kila nchi ukanda huo ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Somalia, Sudani, Sudani ya Kusini, Eritrea na Misri.

Alilipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) , Precision Air na wengine waliofanikisha safari hiyo.

No comments:

Post a Comment