21 August 2012

Mexime aukubali 'mziki' wa Simba B



Speciroza Joseph

KOCHA wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime amekubali matokeo ya kufungwa na Simba B katika mchezo wa fainali ya kombe la SUP8R na kuelekeza nguvu kwenye maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania bara.

Mtibwa juzi ilipokea kipigo cha mabao 4-3 kutoka kwa Simba B, kwenye mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo Mexime, alisema mechi ilikuwa ya ushindani na mshindi ilikuwa lazima apatikane hivyo haikuwa bahati kwao kwa kuwa wachezaji wake wamecheza katika kiwango kikubwa.

"Simba B ni timu nzuri imeonyesha kiwango kinachotakiwa na kuweza kupambana na timu yangu, ulikuwa mchezo wa fainali walitumia makosa yetu wakapata ushindi" alisema Mexime.

Alisema mashindano yalikuwa mazuri upande wao, wamepata nafasi ya kuona viwango vya wachezaji wao wote wapya na wa zamani.

Mexime aliongeza kuwa upungufu ulioonekana kwa timu yake wataanza kuurekebisha mapema kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa ligi kuu.

"Hili tumelimaliza sasa tunaanza maandalizi ya ligi kuu, tutahakikisha sehemu kubwa ya mapungufu yetu tunayarekebisha ili tuanze ligi tukiwa kamili" alisema Mexime.

Nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa na Taifa Stars, aliwapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha ushindani tangu kuanza kwa mashindano hayo na kuwataka waongeze juhudi ili kufanya vizuri kwenye ligi.

No comments:

Post a Comment