21 August 2012

M/kiti CCM: Sitagombea ujumbe NEC



Na Eliasa Ally, Iringa

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, Bw. Seth Moto, amesema hayupo tayari kugombea nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), badala yake atamuunga mkono mbunge wa jimbo hilo, Profesa Peter Msolla, ambaye ameonesha nia ya kugombea.

Alisema uamuzi aliochukua utasaidia kuleta umoja na mshikamano ndani ya chama hicho pamoja na kuondoa makundi yanayoweza kuwagawa wanachi na wanachama.

Bw. Moto aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika Mkutano wa Wenyeviti wa CCM ngazi ya vijiji na kuwaeleza viongozi hao dhamira yake ya kutowania nafasi hiyo.

Alisema mwanachama yeyote wa CCM anapaswa kuwa na mtazamo wa kuwaunganisha wanachama na wananchi badala ya kusababisha malumbano ambayo mwisho wake ni kukigawa chama hicho.

Akizungumzia gari la wagonjwa ambalo alilitoa miaka sita iliyopita na kushindwa kutumika, Bw. Moto, alidai kusikitishwa na kitendo cha gari hilo kushindwa kutumika wakati kuna wananchi wengi ambao wanahitaji kulitumia.

“Gari hili sikulitoa kwa sababu ya kutaka kuwania nafasi yoyote ndani ya CCM, kama Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, imeshindwa kulitumia nitalipeleka katika Wilaya nyingine yenye uhitaji.

“Tufike mahali tuache siasa ndani ya maendeleo ya kweli, kama mimi nilitoa gari kwa CCM, sina maana ya kutaka kugombea nafasi yoyote ya uongozi bali dhamira yangu ni kuimarisha chama,” alisema Bw. Moto.

Alidai kusikitishwa na kitendo hicho kwani gari hilo alilinunua kwa gharama kubwa akiamini litawasaidia wannchi wa Kilolo.

No comments:

Post a Comment