23 August 2012
TFF kuwadhibiti 'wavuta bangi'
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesema litaanza kuwapima wachezaji wanaocheza katika Ligi Kuu na timu ya Taifa, ili kugundua wanaotumia dawa za kulevya (bangi).
Akizungumza Dar es Salaam jana Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema wataanzia katika klabu na kama watapatikana wanaovuta bangi watapewa adhabu kali.
Alisema hivi sasa wanasikia kwa watu kwamba kuna baadhi ya wachezaji wanavuta bangi, lakini hilo hawana ushahidi nalo na ndiyo maana wataanza kuwapima kabla ya mechi kuanza.
"Kwa kuanzia tutawaomba viongozi wa klabu kukaa na wachezaji wao, ili kuwaelimisha madhara ya uvutaji bangi na pia tutalazimika kuwapima kabla kama mchezaji atakataa kupimwa atachukuliwa hatua.
"Tunasikia hawa watoto kuna baadhi wanaovuta bangi, hivyo tunatakiwa kukaa nao na kuwaelimisha nikiwa kama mzazi huwa naumia sana kusikia vitendo hivyo vinafanywa na wachezaji wetu," alisema Tenga.
Alisema baada ya kutoka katika klabu hatua itakayofuata ni kwa wachezaji wa timu ya Taifa, ambao nao wataelimishwa madhara ya uvutaji wa bangi.
Katika hatua nyingine, Tenga alisema kuna umuhimu wa klabu kuwekeza katika soka la vijana wadogo kwa kuwa matunda yake yameanza kuonekana katika timu ya Taifa.
"Kwa kweli kuna haja ya kuwekeza zaidi katika soka la vijana mfano ni hawa vijana akina Frank Domayo, Simon Msuva na hata akina Kapombe (Shomari) wameonekana kucheza vizuri katika michezo ya timu ya Taifa," alisema.
Alisema kwa kulitambua hilo, ndiyo maana shirikisho lake limeamua kutoa baadhi ya vifaa katika michezo mbalimbali ya shule ikiwemo mipira.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment