23 August 2012
BFT yataka wachezaji 'ngangari' wa taifa
Na Mwali Ibrahim
SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania(BFT), limeitaka mikoa kuhakikisha inatoa wachezaji wenye uwezo wa mkubwa wa kushiriki katika mshindano ya taifa yanayotarajia kufanyika Septemba 15 hadi 22, Uwanja wa ndani wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa BFT Makore Mashaga alisema mikoa inatakiwa kulizingatia hilo kwa lengo la kuisaidia BFT kupata wachezaji wazuri watakaounda timu mpya ya taifa.
"Mikoa yote inapaswa kuliangalia hilo, tunataka wachezaji wale wenye uwezo ili kushiriki katika mashindano haya na ndiyo maana tunawasisitiza wafanye kwanza mashindano madogo ya kuwapata na ndipo watutumie majina yao," alisema.
Alisema wanapaswa kujua timu nzuri ya taifa inajengwa kuanzia ngazi ya chini, ambayo ni kutoka mikoani hivyo utekelezaji wao utasaidia kupatikana kwa timu hiyo nzuri itakayokuwa ikitoa upinzani.
Hata hivyo sambamba na kuchagua timu pia BFT imeitaka mikoa kufanya uchaguzi mdogo kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya taifa, na kila mkoa kuwasilisha majina ya viongozi wao wapya sambamba na majina ya wachezaji watakaoshiriki katika mashindano hayo.
Alisema, mikoa mingi imekuwa ikiwatumia makocha kama ndiyo viongozi wao kitu ambacho ni kinyume kwani kila mtu katika chama anatakiwa kukaa katika nafasi yake na sio kuingiliana majukumu na ndiyo maana wanawataka kufanya uchaguzi huo.
Alisema, tayari taarifa zote wanazo na BFT itatoa adhabu kwa mkoa utakaokaidi agizo hilo, kwani wanataka kuona taratibu zinafuatwa kwa ajili ya maendeleo ya ngumi nchini.
Makore aliongeza kuwa katika kulitekeleza hilo ni mkoa wa kimichezo wa Temeke pekee ambao umekamilisha taratibu zote za ushiriki, kwani walishathibitisha majina ya wachezaji, viongozi na makocha kwa maandishi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment