28 August 2012

TFDA yaandaa mafunzo wataalamu wa maabara


Na Heri Shaaban

MAMLAKA ya Chakula na Dawa nchini (TFDA), jana imezindua mafunzo ya siku tatu ya wataalamu wa maabara kutoka nchi 13 za Afrika ambayo yameandaliwa na mamlaka hiyo.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Donan Mmbano, kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi.

Akizungumza  katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Bw. Hiiti Silo, alisema wamepewa fursa ya kuandaa mafunzo hayo kutokana na maabara waliyonayo kuwa na uwezo mkubwa katika mambo ya uchunguzi.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Donan Mmbano, alisema Serikali iliandaa Sera ya Afya kupitia sheria ya maabara ambayo ndio imeunda TFDA.

“Maabara yetu imeimarika na inatarajia kuzinduliwa Novemba mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete, Tanzania inashirikiana na nchi hizi katika chunguzi zake ili kupanua wigo wa kimaabara na malengo yaliyokusudiwa,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Maabara TFDA, Bi. Charys Nuhu, alisema kazi kubwa ya maabara ni upimaji ambapo katika mkutano huo watajifunza mambo mbalimbali na kubadilishana uzoefu.


No comments:

Post a Comment