28 August 2012
Hukumu ya Mtikila yasogezwa mbele
Na Rehema Mohamed
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana imesogeza mbele hukumu ya kesi ya kuchapisha na kusambaza walaka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, hadi Septemba 6 mwaka huu.
Mbele ya Hakimu Frank Moshi, wakili wa Serikali Bw. Genes Tesha, alidai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya hukumu lakini aliomba ipangwe tarehe nyingine kutokana na hakimu anayeisikiliza kesi hiyo Bw. Ilvin Mugeta, kutokuwepo mahakamani.
Alisema Hakimu Mugeta ana majukumu mengine ya kiofisi hivyo anaiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 6 mwaka huu.
Katika kesi hiyo, Bw.Mtikila anadaiwa kuwa kati ya Januari 2009 na Aprili 17, 2010 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya uchochezi, alisambaza kwa umma nyaraka zilizosomeka “Kikwete kuuangamiza ukristo', wakristo waungane kuweka mtu Ikulu”.
Bw. Mtikila katika utetezi wake alikiri kuandaa waraka huo na kusambaza nakala zaidi ya 100,000 nchini na kudai waraka huo si wa uchochezi bali unahusu maneno ya Mungu.
Mmoja wa mashahidi waliomtetea Bw. Mtikila ni mwandishi wa habari Gazeti la Mwananchi Bw. Mpoki Bukuku, ambaye alitoa kielelezo kimoja ambacho ni gazeti la Mwananchi la Agosti 6, 2009 lililokuwa na kichwa cha habari “Mtikila apiga kampeni Kanisani kumpinga JK, achunguzwa na Polisi kumwaga sumu Rais asichaguliwe 2010”.
Akitoa ushahidi wake, Bw. Bukuku aliieleza mahakama hiyo kuwa habari hiyo ilikuwa ikiripoti kilichotokea jijini Mwanza katika mkutano wa Maaskofu ili kuelimisha jamii.
Alidai anaamini habari hiyo haikuwa na tatizo lolote kwa sababu polisi hawajalalamika kwani kama habari ingekuwa na matatizo, huomba radhi au kufanya mapatano mengine.
Bw. Bukuku alisema habari hiyo ilikuwa inahusu mafundisho ya viongozi wa dini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment