02 August 2012
Tanzania yazidi kupotea Olimpiki
Na Amina Athumani
MACHO ya watanzania yamebaki kwa wanariadha katika michezo ya Olimpiki baada ya jana muogeleaji mwingine Magdalena Mushi kuyaaga mashindano hayo yanayoendelea London, nchini Uingereza.
Magdalena aliyaaga mashindano hayo baada ya kumaliza staili huru umbali wa meta 100 akishika nafasi ya saba huku akitumia muda wa dakika 1:05:80 kumaliza umbali huo.
Muogeleaji huyo aliingia uwanjani akiwa na kumbukumbu nzuri ya kuondoshwa kwa muogeleaji mwenzake Amaar Gadiyali juzi aliyeshika nafasi ya 57 kati ya waogeleaji 62 aliyoshindana nao.
Akizungumzia matokeo hayo Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Maselino Ngalioma alisema magdalena hakufanya vizuri ikilinganishwa na Amaar kwa kuwa ameshindwa kutetea muda wake.
Alisema Magdalena alifuzu michezo hiyo ya Olimpiki akitumia muda wa dakika 1:05:25 muda ambao ameshindwa kuutetea katika michezo hiyo ya Olimpiki.
Alisema tofauti na Amaar ingawa hakufanikiwa kuvuka hatua inayofuata lakini amefanikiwa kuvunja rekodi ya muda aliofuzu kuingia kwenye michezo hiyo ya Olimpiki ambapo alifuzu kwa kutumia muda wa dakika 1:03 huku akivunja rekodi ya muda huo kwa kumaliza michezo ya Olimpiki kwa kutumia muda wa dakika 1:01.
Kutokana na matokeo hayo, Tanzania imeshapoteza nafasi tatu hadi sasa baada kwa kutolewa wanamichezo wake watatu bondia Selemani Kidunda na waogeleaji Magdalena na Amaar.
Tegemeo pekee lililobaki kwa watanzania ni katika mchezo wa riadha ambapo Agosti 8, mwanariadha Zakia Mrisho ataingia uwanjani kusaka medali katika mbio za meta 5,000 na Agosti 12 wanariadha Faustine Musa, Msenduki Mohamed na Samson Ramadhani wataingia kusaka medali katika mbio ndefu (Marathon na nusu Marathon).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment