02 August 2012

Braff atua, kufanya shoo kesho



Na Zahoro Mlanzi

MWANAMUZIKI wa miondoko ya Jazz, Malcolm Braff ambaye pia hupiga Piano raia wa Brazil, ametua nchini na anatarajia kufanya maonesho matatu ambapo kesho ataanza kwenye Ukumbi wa Makutano House, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Balozi wa Uswisi nchini, Olivier Chave alisema ujio wa mwanamuziki huo umetokana na ushirikiano wao na Shirika la Maendeleo la Uswisi katika kuendeleza na kukuza maendeleo ya utamaduni.

Alisema kumekuwa na ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na Uswisi kwa muda wa miaka 30 si katika utamaduni ila hata kwenye kuwekeza katika masuala ya uboreshaji wa huduma za afya na uendelezaji wa sekta binafsi.

"Malcolm atafanya onesho Ijumaa (kesho) akiwa pamoja na na Kundi la Bagamoyoni kutoka Bagamoyo ambapo wanapiga muziki wa asili na Jumamosi watapiga Serena ambapo watasindikizwa na Wahapahapa," alisema Chave.

Alisema onesho la mwisho litafanya katika Shule ya Muziki Zanzibar (DCMA) ambalo litashirikisha walimu na wanafunzi ambapo baada ya maonesho hayo watakuwa na mazungumzo na wasanii wa miondoko mbalimbali siku ya Jumatatu.

Alisema ujio wa mwanamuziki huo utasaidia katika kuhamasisha uhusiano wa tamaduni tofauti katika muziki na hatimaye kufungua njia ya muda mrefu kati ya wasanii nchini na wa nje.

Naye Braff alisema anajisikia furaha kupata fursa ya kuja kutumbuiza nchini na kwamba kwa kipindi atakachokuwa nchini ana uhakika atapata tamaduni tofauti kupitia muziki huo.

Alisema tangu aanze kupiga muziki huo amejifunza tamaduni nyingi za nchi kama Senegal na Cape Verde ambapo alikaa nchini kwa vipindi tofauti lakini muda mwingi ameutumia nchini Uswisi.

No comments:

Post a Comment