02 August 2012
Korogwe wamtaka Mbunge wao ajiuzulu
Na Yusuph Mussa, Korogwe
BAADHI ya wakazi wa Korogwe Mjini, mkoani Tanga, wamemtaka Mbunge wao Bw. Yusuph Nassir, kujiuzulu kama itabainika anahusika kushinikiza kufanya biashara na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema pamoja na kuundwa kamati ya kuchunguza madai hayo, wamemtaka Bw. Nassir kwenda kufanya mikutano ya hadhara kwa wananchi wake ili kukanusha madai hayo kama hayana ukweli.
“Kitendo hiki cha mbunge wetu kuhusishwa tuhuma ya kufanya biashara na TANESCO, kimetusikitisha sana, pamoja tuhuma zake kujadiliwa na kamati, tunamtaka aje kutoa maelezo ya kina kwa wananchi wake si kwa waandishi.
“Kama itathibitika alihusika basi ajiuzulu, hakuna haja ya kukaa na mbunge kwa miaka mitano wakati tayari ameingia doa, sisi tulichagua mbunge wa kwenda kututetea, hatumtaki mbunge anayetanguliza masilahi yake,” alisema Bw. Ibrahim Abdillah ambaye ni mwanaharakati na mjasiriamali mjini hapa.
Bw. Abdillah alisema, hivi sasa wanamkumbuka Bw. Joel Bendera, kwani pamoja na kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 15 na baadae Naibu Waziri, bado alikuwa muadilifu, muaminifu na mzalendo kwa Taifa lake.
“Bw. Bendera hajawahi kukutwa na kashfa yeyote inayohusu vitendo vya rushwa au uhujumu uchumi,” alisema.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Stendi Kuu ya Mabasi mjini hapa, Bw. Winfred Tesha, alisema Bw. Bendera aliondolewa kwenye nafasi ya ubunge na viongozi wa chama si wananchi.
Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Bw. Tundu Lissu, mwanzoni mwa wiki aliwataja wabunge saba akiwemo Bw. Nassir kuhusika na kashfa ya rushwa inayoihusisha TANESCO.
Hata hivyo, Bw. Nassir alipoulizwa na waandishi kuhusu tuhuma hizo alikana kuiuzia mafuta TANESCO, akidai yeye ni mfanyabiashara mdogo.
Tuhuma zinazoikabili TANESCO zimesababisha aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika hilo, Mhandisi William Mhando kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi juu ya tuhuma ambazo zinamkabili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment