09 August 2012
Tanzania yazidi kupigwa za 'uso'
Na Amina Athumani
MWANARIADHA Zakia Mrisho, naye ametolewa kwenye michezo ya Olimpiki baada ya kushika nafasi ya 31 kati ya wanariadha 36 waliokimbia mita 5,000 katika michezo ya Olimpiki iliyofanyika jana jijini London, Uingereza.
Katika hatua ya makundi, Zakia alishika nafasi ya 16 kwenye kundi lake lililokuwa na jumla ya wanariadha 18.
Zakia alimaliza mbio hizo akitumia muda wa dakika 15:39:58 muda ambao haukumuwezesha kufika popote katika michuano hiyo mikubwa duniani.
Nafasi ya kwanza katika mbio hizo ilichukuliwa na Tirunesh Dibaba aliyetumia muda wa dakika 14:58:48 na nafasi ya pili ilikwenda kwa Meseret Defar, aliyetumia muda wa dakika 14:58:70 wote wakitokea nchini Ethiopia.
Nafasi ya tatu ilichukuliwa na nchi jirani ya Kenya kupitia kwa Jelagat Viola Kibiwot, aliyetumia muda wa dakika 14:59:31.
Kwa matokeo hayo Zakia, ameongeza idadi ya wanamichezo wanne wa Tanzania walioaga mashindano hayo.
Wachezaji wengine wa Tanzania walioaga michuano hiyo ni bondia Selemani Kidunda, Amar Gadiyali na Magdalena Mushi ambao waliaga siku mbili, baada ya kuanza kwa michuano hiyo Julai 27 mwaka huu.
Kutokana na matokeo hayo Tanzania sasa imebakiwa na nafasi tatu katika mbio ndefu za marathon za kilomita 42.
Wanariadha watakaokimbia mbio hizo ni Samson Ramadhan, Msenduki Mohamed na Faustine Mussa ambao wataingia mzigoni Agosti 12, mwaka huu siku ambayo pazia la michezo ya Olimpiki litafungwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment