27 August 2012
Tanzania yatoka kapa Zone 5 kikapu
Na Amina Athumani
TIMU za Tanzania zilizokuwa jijini Kampala, Uganda kwenye mashindano ya Zone 5, yanayoandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Kikapu (FIBA), zimeondoshwa kwenye michuano hiyo.
Timu hizo ni ABC na Savio kwa timu za wanaume na Jeshi Stars na Don bosco kwa timu za wanawake.
Kwa mujibu wa mtandao wa FIBA Afrika, katika mechi za awali timu za Tanzania, ABC ilifungwa na KCB ya Kenya kwa pointi 95-56, Savio ikifungwa na Urunani ya Burundi kwa 58-51, Jeshi Stars ikilazwa na KPA ya Mombasa kwa 91-38 na mechi ya Donbosco na APR ya Rwanda ikikosa mshindi.
Katika mzunguko wa pili Tanzania iliendelea kuwa vibonde ambapo timu ya Don bosco ilichapwa kwa pointi 92-36 na Eangle Wings ya Kenya, Jeshi Stars ikicharazwa kwa pointi 84-47 na Berco Stars, ABC ikifungwa kwa 85-73 na Dmark Power na Savio ikihitimisha karamu ya kichapo cha pointi 71-59 dhidi ya kyambogo.
Kutokana na matokeo hayo Tanzania imeyaaga mashindano hayo mapema huku Savio ikimaliza michuano hiyo ikiwa na pointi moja ikiwa nafasi ya tatu katika Kundi A na ABC iliyo katika Kundi B ilimaliza michuano hiyo ikiwa nafasi ya nne ikiwa na pointi moja kwa upande wa wanaume.
Kwa upande wa wanawake timu ya Jeshi Stars iliyo katika Kundi A ilimaliza ikiwa nafasi ya nne ikiwa na pointi moja na Don bosco ikimaliza nafasi ya tatu katika Kundi B.
Fainali za michuano hiyo ya Zone 5, imezikutanisha timu za Espoir ya Rwanda na Urunani (bingwa mtetezi) ya Burundi kwa upande wa wanaume na wanawake ikizikutanisha timu za KPA (bingwa mtetezi) na Eagle Wings zote za Kenya.
Fainali hizo zilitarajiwa kuchezwa jana jioni ambapo timu za Tanzania ziliondoka katika jiji la Kampala jana kwa ajili ya kurejea nchini kujipanga na michezo ijayo.
Bingwa wa michuano hiyo kwa wanawake na wanaume atapata nafasi ya kushiriki michuano ya 'FIBA Afro Basketball Afrika' ambayo ni michuano mikubwa itakayozikutanisha timu za Kanda ya Pili, ya Tatu na ya Nne yenye timu kubwa kama za Nigeria , Angola na Misri ambazo tayari zimeshakata tiketi ya kushiriki michuano hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment