27 August 2012

BFT yaomba maandalizi mapema Olimpiki 2016



Na Amina Athumani

SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), limeiomba Serikali kuanza maandalizi mapema ya Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2016 itakayofanyika nchini Brazil, ili kuepuka kujirudia kufanya vibaya kwenye michezo hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Katibu Mkuu wa BFT, Makore mashaga alisema ingawa wao walianza maandalizi tangu mwaka 2009, Tanzania iliporudishiwa uwanachama wake na AIBA (Shirikisho la Dunia la mchezo huo) baada ya kufungiwa kwa miaka miwili, bado ipo haja ya serikali kuwekeza katika maandalizi kwa timu ili ziweze kupata muda mwingi wa kujiandaa.

Alisema ni jambo lisilopingika kwamba michezo hiyo ya Olimpiki ni michezo pekee inayoitangaza nchi kama wanamichezo wake watafanikiwa kufanya vema, hivyo ni wakati wa Serikali kutilia mkazo katika maandalizi ya timu mapema.

Alisema kila mdau anatambua kuwa kufanya vibaya kwa timu za Tanzania kumetokana na maandalizi hafifu na ndio sababu kubwa iliyopelekea wachezaji wa Tanzania kutolewa mapema kwa kuwa walikutana na nchi nyingi zilizojiandaa vya kutosha.

Katibu huyo pia alisisitiza kuwepo kwa kozi nyingi za kimataifa zitakazowafanya makocha wa Tanzania kuwa na upeo mpana wa kuendana na hali halisi iliyopo katika ulimwengu wa sasa ili kutoa mafunzo yatakayoleta tija kwa vijana yatakayolingana na ushindani wa sasa.

Mashaga alisema pia ipo haja ya mchezo wa ngumi kuchezwa mashuleni ambapo kwa sasa mchezo huo bado haujaanzishwa kuchezwa mashuleni kwa kuwa huonekana ni mchezo wa hatari.

"Mfano mzuri timu yetu hii iliyoshiriki mashindano ya Olimpiki walipiga kambi katika chuo cha Black Ford ambacho pamoja na michezo mingine inayochezwa chuoni hapo na ngumi ni mmoja wapo, hivyo na sisi tukiamua kuwafundisha vijana wakiwa shuleni naamini tutapata wachezaji wazuri,"alisema Mashaga.

Katibu huyo pia ameiomba Serikali kuandaa sehemu zitakazokuwa zinajengwa ulingo wa ngumi tofauti na sasa wamekuwa wakiandaa ulingo wa ngumi katika sehemu za baa kinyume na taratibu za michezo.

"Kuna mwaka mmoja tuliendesha mashindano kwenye baa moja pale Mwenge, matokeo yake wachezaji wakarubuniwa, hivyo hii si sahihi kabisa ni vyema kuwepo na uwanja wa ngumi maalum kwa ajili ya mashindano na mazoezi kwa wachezaji,"alisema

No comments:

Post a Comment