10 August 2012
Serikali yaifunda Ngorongoro Heroes
Na Amina Athumani
WACHEZAJI wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes), wametakiwa wasilewe sifa na badala yake kujituma ili kusonga mbele katika mechi ya marudiano ya kuwania tiketi ya kufuzu fainali za vijana kwa Afrika dhidi ya Nigeria.
Katika mchezo wa awali uliopigwa wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam, Ngorongoro Heroes ilifungwa mabao 2-1 na hivyo ili timu hiyo isonge mbele inatakiwa kupata ushindi wa mabao 2-0.
Mechi hiyo ya utachezwa keshokutwa nje ya jiji la Lagos, Nigeria ambapo timu hiyo iliondoka nchini jana mchana kwa ajili ya mchezo huo.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kuikabidhi bendera ya Taifa timu hiyo, Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juliana Yasoda alisema Watanzania wana imani kubwa na vijana hao hivyo wasivimbe vichwa kwa sifa wanazopewa, bali wahakikishe wanaitoa nchi kimasomaso kwa kuiondoa Nigeria katika mechi hiyo.
"Watanzania wengi wana imani na ninyi kwa kuwa ndiyo timu inayojengwa kwa ajili ya timu ya Taifa ijayo, hivyo msivimbe vichwa bali mcheze kwa bidii na kulitetea sifa taifa lenu ili baadaye mje kuwa timu ya Taifa na kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa ambalo ndiyo matarajio ya wachezaji wote," alisema Yasoda.
Naibu huyo amewataka wachezaji hao pia kuwa na nidhamu ya mchezo, kujituma na kuondoa woga uwanjani hata kama watakuwa wakicheza na wachezaji wakubwa wanaocheza soka la kulipwa nje ya Nigeria.
Timu hiyo imeondoka ikiwa na wachezaji 18 huku ikimkosa nyota wake Tomas Ulimwengu, ambaye hatakuwepo katika kikosi hicho ingawa alikuwepo katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam.
Wachezaji walioondoka jana ni Mzee Salum, Atupele Mwaisemba, Alhaji Zege, Simon Happygod, Ramadhan Singano, Hassan Dilunga, Abdallah Hussein, Omega Seme, Frank Raymond, Omari Kheri, Issa Rashid, Hamis Mroki na Hassan Ramadhani.
Wingine ni Leonard Muyinga, Dizzana Yarouk, Samir Ruhava, Baruani Aboubakar na Aish Manula viongozi walioambatana na timu hiyo ni Juma Kizwezwe, John Lymo, Joakim Mshanga, Nassoro Ally, Peter Manyika (kocha wa makipa), Mohamed Rashid (kocha msaidizi), Boniface Wambura (Ofisa Habari), Athumani Kambi na Kocha Mkuu Jacob Michelsen.
Naye Michelsen alisema makosa yaliyojitokeza katika mechi ya awali wameshirikiana vyema na Kocha Tkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen kuyarekebisha na kwamba anaimani na kikosi hicho kitafanya vyema, ingawa mechi hiyo itakuwa ngumu kwa wachezaji wake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment