27 August 2012

Mtoto anusurika kuibwa



Na Mwandishi Wetu, Bukoba

MTOTO wa miaka miwili na nusu, Vanesa Victor, amenusurika kuibwa na watu wasiojulikana waliofika nyumbani kwao wakiwa ndani ya teksi na kumtaka apande ili wampatie soda.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 12:00 jioni katika mtaa wa Kabanga Milembe, Kata ya Hamugembe Manispaa ya Bukoba. Katika tukio hilo ambalo lilivuta hisia za wakazi wengi wa mtaa huo, wanaume wawili
ambao hawajulikani majina yao waliokuwa wakizungumza lugha ya Kiganda, walifika mtaani hapo wakiwa ndani ya gari na kumdang'anya mtoto huyo aingie ndani ya gari.

Kwa mujibu wa majirani walioshuhudia tukio hilo, watu hao waliingia katika nyumba walimopanga wazazi wa mtoto huyo, kwa Bw.Kos Kazinga na kumpatia mtoto huyo ufunguo wa gari ili atangulie kwenye gari.

Mmoja wa shuhuda hao, Bw.Robert ambaye ndiye alimwokoa mtoto huyo na mmoja wa wapangaji katika nyumba hiyo, alisema alilazimika kuwahoji watu hao ambao nao walikuwa katika harakati za kutaka kuwasha gari lao tayari kuondoka na mtoto huyo.

Alipowauliza wanampeleka wapi, bila kujibu lolote walionekana kuwa na wasiwasi na wananchi waliokuwa jirani walianza kurushia gari lao mawe na kuharibika madirisha.

"Unajua hili gari tulilitilia shaka kuwa huenda watu waliokuwemo walikuwa na nia mbaya, kwani walipoulizwa hawakutaka kusema lolote zaidi ya kuzungumza wao wenyewe kwa lugha ya Kiganda, walipoona tunaanza kuwapiga waliamua kuendesha gari kwa kasi wakielekea barabara iendayo Uganda," alisema mmoja wa mashuhuda.

Bw.Mugisha akizungumza na gazeti hili, alisema gari hilo lilianza
kuonekana juzi asubuhi, mtaani hapo likiwa limeegeshwa huku wanaume
wawili wasiowajua wakiwa wanazunguka maeneo hayo hadi hiyo jioni.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwepo kwa watoto wadogo wengi kuanzia mwaka mmoja hadi 15, ambao ikifika jioni hukusanyika pamoja na kuanza kucheza eneo hilo.



No comments:

Post a Comment