09 August 2012

Redondo aikana Azam FC *Adai hana mkataba nayo


Na Zahoro Mlanzi

SUALA la uhamisho wa kiungo, Ramadhani Chombo 'Redondo' kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba linazidi kupamba moto ambapo Klabu ya Azam FC inadai bado mali yao lakini mwenyewe ameibuka na kudai ameshamaliza mkataba na timu hiyo.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Redondo alisema hana mkataba na Azam kwani mkataba wake ulishamalizika tangu Juni, mwaka huu.

"Ninatangaza rasmi kwamba mimi ni mchezaji mpya wa Simba, nimesaini mkataba wa miaka miwili jana (juzi) baada ya mkataba wangu wa miaka miwili nilioingia na Azam FC kumalizika," alisema Redondo.

Akizungumzia kuhusu mkataba wake na Azam, alisema baada ya kumaliza mkataba wake aliiingia makubaliano na timu hiyo kwamba watamuangalia kiwango chake katika michuano ya Urafiki na Kombe la Kagame.

Alidai baada ya michuano hiyo kumalizika hususani ya Kagame, timu hiyo ilikuwa katika mgogoro na ndiyo maana alishindwa hata kuulizia hatma yake, akaamua kujiunga na Simba.

Alipoulizwa kuhusu Azam kudai kwamba bado wana mkataba naye alisema: "Sina mkataba na Azam na kama wana ushahidi kuhusu hilo wawasilishe kwa chombo husika nina imani kila kitu kitakuwa wazi."

Kabla ya Redondo kuzungumza, Makamu Mwenyekiti wa Azam, Said Mohamed wakati wakimtambulisha kocha wao mpya, Boris Kunjak Dar es Salaam jana aliulizwa kuhusu mchezaji huyo ambapo alisema," Bado ni mchezaji wetu na mkataba wake unamalizika Juni, mwakani."

Alisema kama Simba wanamuhitaji mchezaji huyo ni bora wafuate tararibu zinazotakiwa, kama ilivyokuwa kwa Mrisho Ngassa lakini si kutumia njia za panya.

No comments:

Post a Comment