09 August 2012
Azam FC yamtambulisha kocha mpya
Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Azam FC, imemtangaza rasmi Kocha Boris Bunjak 'Boca' kutoka Serbia kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo akirithi mikoba ya Muingereza, Stewart Hall aliyetimuliwa.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kumtambulisha kocha huyo kwa waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Said Mohamed, alisema walipokea maombi ya makocha 19 kutoka sehemu mbalimbali lakini mwisho wa siku wakaamua kumteua kocha huyo.
Alisema wameingia mkataba wa miaka miwili na kocha huyo, ambaye ana uzoefu wa miaka 15 katika kufundisha soka hususani katika bara la Ulaya.
"Tulipokea maombi 19 kutoka kwa makocha wa nchi za Uingereza, Ufaransa na hapa nchini lakini baada ya kufanya mchujo kwa kupitia wasifu wao, uongozi wa Azam ukaridhishwa na wasifu wa Boris na kuamua kumpa kazi," alisema.
Alisema kocha huyo ambaye maarufu kwa jina la Boca kwa mara ya kwanza alifundisha soka katika nchi za Urusi na pia Yugoslavia, Oman na Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu.
Naye Bunjak akizumgumza baada ya kutambulishwa, alisema anashukuru kwa kupata nafasi ya kufundisha soka Afrika hususani Tanzania na kwamba atatumia uzoefu alionao kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri.
Alisema anaifahamu vizuri soka ya Tanzania kupitia kocha wa Simba, Milovan Cirkovic ambaye ni rafiki yake wa karibu kwani wamekutana sehemu mbalimbali kikazi.
"Nina uzoefu katika kazi hii kwa miaka 15, lakini muda wote huo nimefundisha Ulaya na kikubwa ninachohitaji katika timu yangu ni nidhamu kwani ndicho kitu ninachokipa kipaumbele," alisema Bunjak.
Kocha huyo ana leseni ya juu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA) na pia kabla ya kuwa kocha amewahi kucheza soka katika timu za nyumbani kwao za FK Sloga, FK Vozdovac na zingine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment