22 August 2012
Rais Kagame aipeleka Yanga Rwanda
Na Zahoro Mlanzi
MABINGWA wa Kombe la Kagame, Yanga imeondoka nchini jana mchana kwenda Rwanda kwa ajili ya ziara ya kimichezo ya wiki moja, ambapo itacheza na Rayon Sports na Police Force za nchini humo.
Timu hiyo imeondoka na wachezaji wote waliowasajili kwa ajili ya Ligi Kuu Bara, inayotarajiwa kuanza kutimia vumbi Septemba 15, mwaka huu ikiwa imesogezwa mbele kwa wiki mbili, ziara hiyo ni mwaliko wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo Yusuph Manji, alisema mbali na mwaliko wa Rais Kagame, pia Rais Jakaya Kikwete amewaalika na anahisi itakuwa kupongezwa kwa kutwaa ubingwa.
"Ukiachana na mwaliko wa Kikwete, pia tumepata mwaliko kutoka kwa Rais Kagame, ambaye ametualika nchini kwake na tunaondoka mchana huu na kikosi chote na viongozi wetu kati ya watano mpaka saba," alisema Manji.
Alisema anamshukuru Rais Kagame kwa mwaliko huo, ambapo kwa mujibu wa ratiba yake watakutana naye leo huku pia wakimshukuru Rais Kikwete kwa kuwapa heshima hiyo na kwa kutambua kwake mchango wa timu yake katika kuinua soka la Tanzania.
Alisema wanamuahidi Rais Kikwete, mara watakaporejea kutoka Rwanda watahakikisha watakwenda kumuona kama ratiba yake itakavyokuwa inaruhusu.
Aliwwashukuru mashabiki na wanachama wa Yanga kwa ushirikiano walioutoa wakati wa Kombe la Kagame na kwamba mshikamano huo uendelee mpaka kwenye ligi.
Naye Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesiga alipoulizwa kuhusu timu watakazocheza nazo Rwanda, alisema: "Wenyeji wetu wametuambia tutacheza mechi tatu dhidi ya Rayon Sports, Police Force na nyingine watatuambia tukifika huko na pia tunafanya mpango wa kufungua tawi letu jijini Kigali".
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment