RAIS Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kuwafichua wabadhirifu fedha za miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na wale wanaotumia vibaya rasilimali za mfuko huo.
Aliwataka wananchi kushirikiana na viongozi wa TASAF ili kubuni miradi mbalimbali ambayo itawaletea maendeleo ya haraka na kuboresha huduma za kijamii.
Rais Kikwete aliyasema hayo mjini Dodoma jana wakati akizindua awamu ya tatu ya miradi inayotekelezwa na mfuko huo nchini.
“Miradi hii ya TASAF ni kwa ajili yetu sisi na watoto wetu, ndugu pamoja na jamaa hivyo kama tutaitunza, tutakuwa na msingi imara wa kujenga Taifa letu na kushinda vita dhidi ya adui wa maendeleo.
“Wananchi hakikisheni mnafuata maekezo ya wataalamu na viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali, washiriki wa maendeleo na viongozi wa TASAF, isaidieni Serikali ili iweze kufikia malengo iliyojiwekea katika awamu hii,” alisema.
Aliwataka viongozi hao kuongeza ufanisi na maarifa ya utendaji kazi wao, kusimamia fedha, rasilimali, kujenga uwezo wa kutekeleza miradi husika na kubuni vyanzo vipya vya kupata fedha za kuendeleza miradi hiyo.
Rais Kikwete alisema, utekelezaji wa Awamu ya Pili ya TASAF ulikuwa na mafanikio makubwa kwani jumla ya miradi 11,572 ilitekelezwa kati ya hiyo, 4,294 ilikuwa ya huduma za jamii, 1,405 ya ujenzi na 5,875 ya makundi maalumu.
Alisema miradi hiyo iligharamiwa na Serikali ambayo ilitoa sh. bilioni 32.2 ambapo washirika wake wa maendeleo ambao ni Benki ya Dunia ilitoa sh. bilioni 322 ambazo ni mkopo wa masharti nafuu.
“Washirika wetu wengine nao walituongezea nguvu kwa kuchangia sh. bilioni 72, wananchi walitoa fedha, rasilimali na nguvu kazi ambazo thamani yake inakadiriwa kuwa zaidi ya sh. billioni 20.2,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa, awamu ya tatu ya TASAF itatekelezwa kwa miaka 10 katika vipindi viwili vya miaka mitano mitano na itatoa mchango mkubwa ili kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, kukuza uchumi na kupunguza umaskini Zanzibar, miradi ya elimu, afya na maji ili kuondoa umaskini wa kipato.
“Utekelezwaji wa awamu hii, utazisaidia kaya nyingi maskini kupiga hatua ya maendeleo na kutoka kwenye maisha ya utegemezi, nampongeza Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa, kwa ubunifu wake wa kuanzisha mfuko huu,” alisema.
No comments:
Post a Comment