17 August 2012

Wapendekeza ujenzi wa barabara chini ya ardhi




Na Grace Ndossa

SERIKALI imeombwa kupanga Mpango wa muda mrefu wa kujenga barabara inayopita chini ya ardhi Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ili kupunguza makali ya kona zenye kutisha kwa usalama wa wakazi wakiwemo wageni mbalimbali.


Mwito huo ulitolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali Lianalojishughulisha na Harakati za Kupunguza Ajali na Umaskini (APEC) Bw. Respecius Timanywa alipokuwa anatoa elimu ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki mkoani Tanga.

Alisema kuwa,  kwa sasa wameweza kutoa elimu kwa zaidi ya vijana 3,000 katika Wilaya ya Tanga Mjini, Muhenza, Korogwe, Lushoto na Handeni.

"Mpango wa muda mrefu wa kuunda barabara ipitayo chini ya ardhi katika Mkoa wa Tanga Wilaya ya Lushoto ili kupunguza makali ya kona zenye kutisha kwa usalama wa wakazi na wageni unahitajika," alisema Bw. Timanywa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bw. Muhingo Rweyemamu akifunga mafunzo ya waendesha pikipiki 760 wa wilaya hiyo alisema, vurugu za ajali za pikipiki zimepungua kwa kiasi kikubwa baada ya kupatiwa mafunzo madereva hao.

"Shirika hili linafanya kazi nzuri kwani wanatusaidia kutekeleza ahadi za  Serikali, hivyo wanatakiwa kupatiwa gari lenye uwezo wa kwenda vijijini kuendelea kutoa mafunzo sehemu mbalimbali," alisema Bw.Rweyemamu.

Naye Mkuu wa Polisi Mkoa wa Tanga Kamishina Msaidizi Bw. Constantine Massawe alisema matukio ya uhalifu yamepungua baada ya kuanzishwa vikundi vya ulinzi shirikishi na waendesha pikipiki.

Naye Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo, Bw. Abdi Isango alisema mafunzo ya APEC yamesaidia kupunguza ajali za barabarani ambapo Tanga Mjini ajali za pikipiki zimeshuka kutoka 40 kwa wiki mpaka nane, Muheza zimeshuka kutoka 64 hadi 12, Korogwe 75 hadi 14, Lushoto zimeshuka kutoka 32 hadi mbili na Handeni zimeshuka kutoka 80 hadi tatu.

No comments:

Post a Comment