16 August 2012
Poulsen amsuka upya Boban
Na Mwandishi Maalumu, Botswana
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa, (Taifa Stars) Kim Poulsen ameanza kazi ya kutengeza washambuliaji katika kikosi chake akianzia na Haruna Moshi 'Boban'.
Kocha huyo ameamua kuinoa safu hiyo, ili timu hiyo iweze kuwa na hazina ya washambuliaji wenye uchu wa kupachika mabao.
Stars ambayo inadhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, ipo jijini hapa ambapo jana usiku ilitarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Botswana 'Zebras' ikiwa ni maandalizi na kujiandaa na mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka 2018.
Akizungumza na Boban (juzi) usiku baada ya mazoezi ya timu hiyo mjini hapa Poulsen alimwambia: “Wewe ni mchezaji mzuri na una uwezo wa kuisaidia timu na kuanzia leo (juzi), ninakupa jukumu la kucheza kama mshambuliaji.
“Nakupa kazi hii kwa sababu nimegundua ukicheza kama mshambuliaji, unaweza kufunga magoli mengi kuliko ukicheza kama kiungo, sababu ya msingi ni kwamba ninataka uzibe pengo lililoanza kujitokeza, baada ya Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na John Bocco kukosekana,” aliongeza.
Katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa zaidi ya dakika 15, Poulsen alimwambia Boban kwamba katika kikosi chake yeye ndiye mchezaji mwenye uzoefu kuliko wengine na amegundua hata wachezaji pia wanamuheshimu na wanashirikiana vizuri, ndani na nje ya uwanja.
"Mbali na hilo wewe ni kati ya wachezaji wanaotambua wajibu wao ndani na nje ya Uwanja, sawa Moshi,” alimwambia.
Baada ya Poulsen kuzungumza na Boban, alisema kuanzia sasa mchezaji huyo atakuwa akicheza kama mshambuliaji katika timu hiyo na si kama kiungo mshambuliaji.
Alisema Boban ni mchezaji mwenye akili na asiye na papara anapokuwa ndani ya eneo la kufunga na kwamba ni kati wachezaji wachache, wanaocheza nafasi ya kiungo wenye uwezo wa kufunga.
Kwa upande wake Boban, alisema amekubaliana na uamuzi huo kwa sababu kocha wake amegundua akicheza kama mshambuliaji ataisaidia timu zaidi kuliko akiwa kiungo, hivyo yeye kama mchezaji hana tatizo na atafuata ushauri huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment