27 August 2012
Polisi wafichua hujuma ya sensa *Wabaini uwepo wa kikundi kilichopanga kuivuruga
Stella Aron na Anneth Kagenda
JESHI la Polisi nchini limedai kubaini uwepo wa kikundi cha watu ambao wanajipanga kuvuruga Sensa ya Watu na Makazi ambayo imepangwa kuanza usiku wa kuamkia Agosti 26 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Bw. Paul Chagonja,
alisema polisi wamejipanga kuzuia kusudio la kikundi hicho.
Alisema Jeshi la Polisi halipo tayari kuwavumilia watu ambao watahusika kuvuruga sensa ambayo inafanyika kwa mujibu wa sheria kutokana na umuhimu wake.
“Mtu yeyote ambaye atakamatwa kwa kosa la kuhujumu sensa, atashtakiwa na kufungwa jela miaka mitano au kulipa faini, mbinu zao za kuvuruga sensa zitashindwa kwani tumejipanga vizuri.
“Hatutawavumilia watu wachache au kikundi cha watu ambao watawashawishi wenzao wasishiriki au wanaotaka kutumia mwanya huo kuvuruga amani na usalama wa nchi,” alisema.
Bw. Chagonja alisema jeshi hilo halipo tayari kuona kikundi chochote kikiwatisha, kuwazuia watu wengine wasishiriki sensa au kuwaletea fujo makarani na wasimamizi ili wasitimize wajibu wao.
“Sensa inatarajia kuanza usiku wa kuamkia kesho na lengo kuu ni kujua idadi ya watu nchini pamoja na kukusanya taarifa muhimu kama umri, jinsi, mahalali wanapoishi, kiwango cha elimu, hali ya ajira, uzazi, vifo, makazi na taarifa nyingine za maendeleo ya nchi.
“Kutokana na umuhimu wa jambo hili, Jeshi la Polisi wanawaomba wananchi wote kushiriki kikamilifu bila hofu wala wasiwasi wa aina yoyote, ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote ili kuhakikisha linakamilika kwa amani na utulivu,” alisema Bw. Chagonja.
Aliongeza kuwa, hadi sasa tayari jeshi hilo limewatia mbaroni baadhi ya watu mikoani waliobainika kuhamasisha wananchi wasishiriki sensa.
Aliwashukuru viongozi wa dini, wanasiasa, vyombo vya habari na taasisi mbalimbali kwa jitihada zao za kutoa elimu ya sensa kwa wananchi ili Serikali iweze kutimiza malengo yake.
Wakati huo huo, wito umetolewa kwa wanasiasa nchini kuacha kuwashinikiza baadhi ya Waislamu wasishiriki sensa kwani kufanya hivyo ni kutaka kuivuruga Serikali na mipango yake ya maendeleo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Islamic Peace Foundation, Shekhe Sadiki Godigodi, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Shekhe Godigodi alisema baadhi ya wanasiasa wanatumika kuwashawishi Waislamu wasikubali kuhesabiwa wakati suala la maendeleo linawahusu wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Sisi viongozi wa jumuiya, taasisi mbalimbali na Mabaraza ya Kiislamu kwa umoja wetu, tunawaonya baadhi ya wanasiasa wanaofanya vitendo hivi waache mara moja kuanzisha migogoro isiyo ya lazima na tija kwa nchi yetu,” alisema Shekhe Godigodi.
Aliongeza kuwa, Serikali inapopanga mipango yake ya maendeleo haiangalii dini, kabila wala rangi na kuwaonya wanasiasa kuacha tabia hiyo kwani inaweza kuvuruga amani iliyopo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment