27 August 2012
Katibu CHADEMA Morogoro ajiuzulu
Na Lilian Justice, Morogoro
KATIBU wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani Morogoro, Bw. Abeli Luanda, jana ametangaza kujiuzulu wadhifa huo kwa madai ya kutoridhishwa na utendaji mbobu wa chama hicho ngazi ya Mkoa na Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa, Bw. Luanda alisema ameamua kujiuzulu kutokana na upepo mbaya wa kisiasa uliopo ndani ya chama hicho na kukosa ushirikiano wa Mwenyekiti wa Mkoa tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo.
Sababu nyingine ni kudharauliwa kwa viongozi waanzilishi wa chama hicho ambao ndio wamekilea na kuhakikisha idadi ya wanachama mkoani humo inakua siku hadi siku.
“Kimsingi sababu zipo nyingi, nyingine ni kupisha agenda ya siri ndani ya Operesheni Sangara (M4C), ambayo imelenga kuwaondoa baadhi ya viongozi wa Mkoa huu na Wilaya zake,” alisema.
Aliongeza kuwa, CHADEMA wameshindwa kutekeleza katiba yake hasa ibara ya saba ambayo inaelezea namna ya kuwapata viongozi ndani ya chama hicho.
Alilalamikia kitendo cha uongozi wa chama hicho Taifa kuweka viongozi na wanachama wapya bila kuangalia mwenendo wao kama wanastahili kupewa uongozi au kupokelewa.
Bw. Luanda hakuweza kusema ni chama gani cha siasa ambapo atajiunga nacho mbali ya kuwepo tetesi za kutaka kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment