23 August 2012

Ochieng, Mudde waipasua kichwa Simba



Na Zahoro Mlanzi

BAADA ya kuonekana kuna kusuasua kwa Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) za wachezaji Pascal Ochieng na Mussa Mudde, Klabu ya Simba, inatarajia kwenda nchini Kenya kukamilisha suala hilo kwa kuonana na timu za wachezaji hao pamoja na Shirikisho la Soka nchini humo.


Wachezaji hao ni miongoni mwa wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo msimu huu, wakitokea timu ya AFC Leopards na SOFAPAKA kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao cha Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa timu hiyo, Ezekiel Kamwaga alisema wamesubiri kwa muda mrefu ITC za wachezaji hao kutua nchini, lakini imekuwa ngumu na hawana taarifa zozote juu ya suala hilo wakati taratibu za usajili wamezikamilisha.

"Kutokana na hali hiyo, klabu imeamua kumtuma Katibu wetu, Evodius Mtawala kwenda jijini Nairobi kushughulikia suala hilo kwa kuonana na viongozi wa timu na chama cha soka kujua kinachoendelea," alisema Kamwaga.

Pia alisema tayari wameshapokea ITC ya mshambuliaji wao, Daniel Akkufo, hivyo ni ruksa sasa kumtumia katika mashindano yoyote na tayari yupo jijini Arusha akiendelea na mazoezi na wenzake.

Akizungumzia kwa ujumla maandalizi ya timu hiyo kwa ajili ya ligi na Ngao ya Jamii, Kamwaga alisema timu inaendelea vizuri na mazoezi Arusha na kwamba wachezaji wote wapo vizuri kiafya isipokuwa Mudde ambaye anasumbuliwa na kifundo cha mguu na Emmanuel Okwi yupo katika timu ya Taifa ya Uganda 'The Cranes' inayojiandaa na mechi dhidi ya Botswana.

Alisema kwa mujibu wa Kocha, Milovan Cirkovic amehitaji mechi za kirafiki za timu za nyumbani ambapo suala hilo linashughulikiwa na uongozi wa juu.

Mbali na hilo, pia alizungumzia kuhusu kusogezwa mbele kwa ligi hiyo ambapo alisema imewagharimu kutokana na awali walijua wangetoka jijini humo leo kurudi Dar es Salaam kwa ajili ya mechi yao dhidi ya Azam FC ya Ngao ya Jamii.

"Kutokana na mabadiliko hayo, inatulazimu sasa tuendelee kubaki Arusha kitu ambacho kitatufanya gharama za maandalizi ziongezeke, lakini pamoja na hayo pia itatoa nafasi za timu kujiandaa kwa muda mrefu," alisema Kamwaga.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi kwa wachezaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), amekubali kuendelea kuwa mjumbe wa kamati hiyo kama alivyoombwa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga.

Kwa mujibu wa Kamwaga, alisema Mwenyekiti wake amekubaliana na uamuzi wa Tenga kwa moyo mkunjufu bila masharti yoyote na hiyo imetokana na Rage kufanya mazungumzo binafsi na Tenga.

Alisema ana imani na wajumbe wa kamati hiyo na kwamba atahakikisha anaitumikia kamati hiyo kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa.

No comments:

Post a Comment