23 August 2012

Yanga wapata mapokezi makubwa Rwanda *Kutinga Ikulu kwa Kagame leo



Na Elizabeth Mayemba

MABINGWA wa Kombe la Kagame Yanga, juzi walifika salama nchini Rwanda na kupata mapokezi makubwa kwa mashabiki wa timu hiyo waishio nchini humo, ambapo leo mchana wanatarajia kutinga Ikulu kwa Rais Paul Kagame.

Timu hiyo iliondoka juzi jioni ikiwa na wachezaji wote waliosajiliwa kwa ajili ya ziara ya wiki moja ya kimichezo, ambapo wamefikia katika hoteli ya Laparis nje kidogo ya jiji la Kigali,Rwanda.


Akizungumza kwa simu jana kutoka Rwanda, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Abdallah BinKleb alisema hawakutarajia kupata mapokezi makubwa kama yale, hali ambayo kwao ilikuwa ni kama wamestukizwa.

"Kwa kweli ile ilikuwa ni suprise kwetu kwani hatukutarajia kupata mapokezi makubwa kama yale, mashabiki wetu wa huku walikodi mabasi matatu kwa ajili ya kuja kupokea msafara wetu," alisema BinKleb

Alisema jana walikuwa na wenyeji wao kwa ajili ya kutembelea makumbusho mbalimbali, ambapo leo mchana watakuwa Ikulu ya Rwanda kwa ajili ya mwaliko waliopewa na Rais Paul Kagame.

BinKleb alisema kesho wanatarajia kucheza na Rayon Sports ya huko na Jumapili watacheza na Polisi ya huko.

Akizungumzia kuhusu beki wao Mkongo, Mbuyu Twite BinKleb alisema mchezaji huyo alikuwa kwao Kongo kwa ajili ya kujiandaa na walimtarajia jana usiku angekuja kujiunga na wenzake akitokea kwao.

"Twite anajua kama tupo huku Rwanda baada ya kumpa taarifa na tulitarajia leo (jana) usiku angetua na kuungana na wenzake," alisema.

No comments:

Post a Comment