24 August 2012

NBC kutumia fursa za kiuchumi kupiga hatua


Na Godfrey Ismaely

BENKI ya NBC, imesema licha ya changamoto zilizopo katika ushindani wa kibiashara na uwekezaji, bado kuna fursa nyingi za masoko ambapo hali hiyo inaweza kuifanya benki hiyo iweze kujiimarisha na kukua zaidi kibiashara nchini.


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Marius Alberts, aliyasema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana wakati akifafanua mtazamo wa utendaji kazi wa benki hiyo kwa miezi sita ambao unaishia Desemba mwaka huu.

“Mbali na hasara ambayo imejitokeza katika robo ya pili ya mwaka sh. bilioni 20.2, tunaamini tunaweza kumaliza mwaka vizuri na ikiwezekana kuifuta harasa hii kwa miezi sita ya kwanza,” alisema.

Aliongeza kuwa, hasara hiyo inaweza kuhusishwa na upotevu wa sh. bilioni 13.9,ambapo hali hiyo imesababishwa na matatizo ya kiufundi mwaka mwaka 2008 hadi Juni 2012.

“Kati ya sh. bilioni 13.7 ambazo zinatolewa na kampuni mama nje ya nchi, hayo ni matokeo mabaya kwa miezi sita na hayatatokea tena,” alisema Bw. Alberts na kuongeza kuwa, hiyo ni tathimini ya mizania iliyofanywa na benki hiyo katika kipindi hicho.

Alisema mizania hiyo ilifanywa kupitia akaunti zote ambapo lengo lao ni kuangalia mbele zaidi ili kuhakikisha ndani ya miezi sita mambo yanakuwa mazuri zaidi.

Hata hivyo, NBC ni kati ya benki zenye uzoefu wa zaidi ya miaka 45 nchini ambayo huwa inatoa huduma mbalimbali za kifedha.

“Benki yetu inatoa huduma za benki za kawaida kupitia ATM, pia tuna matawi 53, na inatoa huduma za 'Visa na MasterCard' na kuajiri zaidi ya wafanyakazi 1,387, hadi kufikia Juni 2012,” alisema.

Bw. Alberts aliongeza kuwa, kupitia taarifa hiyo NBC ni taasisi yenye nguvu nchini kutokana na bidhaa zake zenye ubora na huduma kababambe kwa Watanzania.

“Sisi ahadi yetu ni kutoa huduma bora kwa wateja kupitia wafanyakazi wenye ari, tunawashukuru wadau wetu wote kwa kutuunga mkono zaidi ya miaka 45 iliyopita.

“Nawahakikishia kuwa, sisi tunawatekelezea huduma wanazotaka kila mahali,” alisema Bw. Alberts.


No comments:

Post a Comment