16 August 2012
Mwanafunzi abakwa, auawa kwa kunyongwa
Na Luppy Kung’alo, Jeshi la Polisi Dodoma
MWANAFUNZI wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Hogolo, (jina tunalo), mwenye umri wa miaka 14, ameuawa kwa kunyongwa baada ya kubakwa na mwili wake kufukiwa katika shimo nyuma ya nyumba yao karibu na choo.
Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Zelothe Stephen, alisema tukio hilo limetokea Agosti 11 mwaka huu, saa mbili asubuhi katika Mtaa wa Ikulu, Kijiji cha Hogolo, Kata ya Hogolo, Tarafa ya Zoisa, wilayani Kongwa.
“Uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha mauaji haya ni wivu wa mapenzi kwani marehemu alikuwa amevunja uhusiano na mpenzi wake wa muda mrefu na kuanzisha uhusiano na kijana mwingine.
“Hivi sasa tunawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji hayana ili kufanikisha uchunguzi wa awali, tunamshikilia mpenzi mpya wa marehemu, yule wa zamani hajulikani alipo baada ya kukimbia,” alisema Kamanda Stephen.
Alisema katika tukio hilo, kaka wa marehemu ambaye anashikiliwa na jeshi hilo alidai kusikia purukushani zikitokea usiku wa tukio lakini hakuweza kutoka usiku nje ili kuangalia kilichotokea.
Kamanda Stephen alisema marehemu alikuwa akiishi na babu pamoja na bibi yake ambapo siku ya tukio hawakuwepo nyumbani walikuwa katika vijiji jirani.
“Bibi wa marehemu alikuwa Kongwa ambako alikwenda kujenga makaburi na babu yake alikuwa Kijiji cha Banyi Banyi ambako alikwenda kutemebelea wagonjwa,” alisema.
Wakati huo huo, gari lenye namba za usajili T 750 AEU, aina ya Toyota Chaser, ambalo lilikuwa likiendeshwa na Bw. Kenedy James (48), mkazi wa Mpwapwa, liliacha njia, kupinduka na kusababisha kifo cha Salum Kaduma (13), ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ye Sekondari ya Mpwapwa.
Kamanda Stephen alisema, ajali hiyo ilitokea juzi saa tatu asubuhi katika eneo la Kisima, Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma.
“Uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha ajali ni kupasuka kwa magurudumu mawili ya upande wa kulia hivyo kusababisha gari kuacha njia na kupinduka,” alisema Kamanda Stephen.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment