16 August 2012
Wadau waiponda bajeti ya elimu
Willbroad Mathias na Faida Muyomba
WADAU wa elimu nchini, wameiponda Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka wa fedha 2012/13 ambayo imesomwa bungeni mjini Dodoma jana na Waziri wake, Dkt. Shukuru Kawambwa.
Walisema makadirio hayo hayana mashiko na hayalengi kutatua tatizo lililopo katika sekta hiyo kwa sasa bali ni mwendelezo wa hadithi kama ilivyo katika bajeti zilizopita.
Wadau hao waliyasema hayo Dar es Salaam jana katika warsha ya siku moja iliyolenga kujadili bajeti ya Wizara hiyo ili kuona kama itasaidia kuleta madadiliko ya elimu nchini ambayo iliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la HakiElimu.
Akiwasilisha mada katika warsha hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Kitila Mkumbo, alisema hotuba hiyo ina kasoro nyingi hasa kwenye uwiano wa idadi ya wanafunzi wanaotakiwa kufundishwa na mwalimu katika darasa moja.
Alisema katika baadhi ya vijiji, shule moja ina mwalimu mmoja au wawili lakini Serikali haijasema hatua ambazo watachukua ili kumpunguzia mwalimu mzigo na kuinua kiwango cha elimu.
Aliongeza kuwa, pia hotuba hiyo haijazungumzia mgomo wa walimu na wanafunzi wa vyuo vikuu wakati akieleza changamoto mbalimbali zinazoikabili Wizara yake.
“Kitendo cha Waziri kutozungumzia mgomo wa walimu, kinaweza kusababisha kiwango chetu cha elimu kuzidi kuporomoka, matatizo ya walimu yasipopatiwa ufumbuzi ni sawa na kuchezea elimu,” alisema Dkt. Mkumbo.
Akizungumzia chanzo cha migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, alisema inachangiwa na mfumo mbovu wa utoaji mikopo na kuishauri Serikali kutafuta utaratibu mwingine ili walengwa waweze kupata mikopo hiyo kwa wakati.
Aliipongeza Serikali kwa kuanzisha Bodi ya Taaluma ambayo itasaidia kushughulikia matatizo mbalimbali ya walimu na wahadhiri.
Naye Dkt. Adolf Mkenda, kutoka Idara ya Uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema hotuba hiyo haina uchambuzi yakinifu ili kinachokusudiwa kiweze kueleweka.
Alisema sehemu kubwa ya fedha katika bajeti hiyo ni kwa matumizi ya kawaida badala ya kujikita katika shughuli za maendeleo ya elimu nchini.
Alisema mbali na kasoro hiyo, bajeti hiyo pia haijataja mikakati ya kuwaandaa walimu wengi ili waweze kutoa elimu bora.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment